Header Ads

MAPIPA 200 YALIYOSHEHENI KEMIKALI YAKAMATWA MWANZA

Image result for mwanza

Katika kulinda usalama wa afya za binadamu na matumizi ya dawa za kulevya nchini Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya  (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imekamata mapipa 200  yenye kemikali bashirifu inayosadikiwa  kuwa ni ethyl alcohol.

Kamishina wa Ukaguzi na Sayansi Jinai, DCEA,  Bertha Mamuya alitoa taarifa  jana Desemba 22 inayoeleza kuwa kiasi hicho kilikamatwa Desemba 13, 2017 katika kivuko cha Kigongo Ferry kilichopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

Bi.Bertha Mamuya lisema kemikali hiyo ilikuwa ikisafirishwa na kampuni ya Mwanza Lake Line Industiries kwenda nchini DRC Congo,na gari linalomilikiwa na kampuni ya Mhili ya jijini Mwanza.

“Gari hili lilikamatwa likiwa halina nyaraka zinazoruhusu kisheria kusafirisha kemikali hizo,kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria namba tatu ya kemikali za viwanda na nyumbani ya mwaka 2003, na sheria ya dawa za kulevya namba tano ya mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2017.” Alisema Bi.Bertha Mamuya.

Bi. Bertha Mamuya aliongezea kuwa kampuni hiyo ya Lake Line ikiwa inatambua kuwa imekiuka utaratibu za kujihusisha na kemikali, Desemba 14, iliidanganya mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuomba kibali cha kutaka kusafirisha kemikali bashirifu na kupewa kibali hicho wakati tayari gari lenye kemikali hizo lilikuwa limeshakamatwa.

Aidha, uchunguzi wa awali umeonyesha  kuwa kampuni hiyo imewasilisha  taarifa za uongo katika mamlaka mbalimbali za udhibiti, ikiwamo kiasi cha kemikali kilichokuwa kinasafirishwa na magari yaliyotakiwa kuisafirisha.

Hivyo Bi.Bertha Mamuya alisema kuwa DCEA kwa kushirikiana na mamlaka husika na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusu kampuni hiyo na kwamba uchunguzi utakapokamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika ili kukomesha usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya.

No comments