Header Ads

MWANZA: MWANAUME AMUUA MKEWE KISHA NA YEYE KUJINYONGA

Taarifa kutoka jeshi la polisi mkoa wa Mwanza imeeleza kuwa mwanaume mmoja anatuhumiwa kumuua mkewe kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali sehemu za mwili wake kisha na yeye mwenyewe kujinyonga hadi kufa kwa kutumia waya wa umeme wilayani Magu mkoani humo ambapo kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi, Ahmed Msangi amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa mtu huyo ametambulika kwa jina la John Ntemi (23) mkazi wa Kijiji cha Mahaha ambaye anatuhumiwa kwa kumuua mkewe Casta Edward.

Hata hivyo kamanda Msangi amesema inadaiwa watu hao wawili walikuwa wanaishi peke yao na kabla ya tukio hilo kutokea wanandoa hao walikuwa wakiishi kwa amani na upendo bila ya mgogoro wa aina yeyote kati yao, lakini ilipofikia Machi 26, 2018 majira ya saa 6:00 mchana mwenye nyumba waliyokuwa wamepanga alipita karibu na maeneo ya nyumba yao ndipo alipoona damu chini ya mlango, na kuweza kutoa taarifa kwa majirani pamoja na Jeshi la Polisi.

Kamanda Msangi ameongeza kuwa polisi walipofika katika eneo la tukio waliweza kukuta mwili wa mwanamke ukiwa mlangoni ndani ya nyumba eneo la tukio huku ikionesha miburuzo ya damu toka chumbani hadi mlangoni na mlango ukiwa umefungwa kwa kufuli.

Uchunguzi wa awali unaonesha mauji hayo yalitekelezwa usiku wa Machi 25, 2018 kutokana na kuwepo kwa mvua kubwa katika kijiji hicho kiasi kwamba majirani wasingeweza kusikia kilichokuwa kikiendelea ndani  ya nyumba ya wawili hao.

Miili hiyo imechukuliwa na jeshi la polisi na  kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

No comments