Header Ads

WAZIRI WA NISHATI AMEAGIZA WANAKIJIJI WANAUGANISHIWA UMEME BILA KUJALI HADHI ZA NYUMBA ZAO

   Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameagiza  kuwa wanakijiji wa Mbuyuni kata ya Oljoro  wanafikiwa na nishati ya umeme kijiji kwa kijiji na kitongoji kwa kitongoji bila kubagua hadhi ya makazi na nyumba zao.

   Waziri Kalemani ameyasema hayo hayo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa umeme vijiji - REA eneo la Mbuyuni wilayani Arumeru Mkoani Arusha Machi 20, 2018.
       
     Waziri Kalemani ameliagiza shirika la umeme TANESCO mkoa wa Arusha  kupitia wakala wa umeme vijijini-REA kuhakikisha linawaunganishia umeme wananchi wote bila kujali hadhi za nyumba zao wanazoishi.      

     Aidha Waziri Kalemani amesisitiza kuwa umeme unawekwa kwa kila mwananchi anayehitaji na mwenye uwezo wa kulipia gharama za kuunganishiwa umeme hata kama nyumba yake ni ya udongo na imeezekwa kwa nyasi.    
 
     "Sitaki kusikia mmeacha nyumba kwa sababu hali duni ya nyumba, hali ya nyumba ya mtu haiwahusu" alisema Kalemani

  Waziri Kalemani  aliongeza na  kuwataka wananchi hao kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme kiasi cha shilingi 27,000 tu ili aweze kuunganishiwa umeme na si vinginevyo na kama mwanachi atatozwa zaidi ya hapo  atoe taarifa kwa viongozi wa  ngazi ya wilaya na mkoa.

     Hata hivyo Waziri huyo ameagiza umeme uunganishwe ndani ya siku saba baada ya mwananchi  kukamilisha taratibu za malipo, na kuwataka wananchi kulinda miundombinu ya umeme katika maeneo yao na kujenga uzio kwenye transfoma ili kuepusha athari zitokanazo na miundombinu hizo.

       Kwa upande wake Meneja wa TANESCO mkoa wa Arusha Gasper Msigwa amesema kuwa REA III kwa kipindi cha awamu ya kwanza itawaunganishia nishati ya umeme wateja wapatao 6,000 katika maeneo 58 ya mkoa wa Arusha, mradi utakao gharimu shilingi bilioni 9.3.
    Akitoa taarifa ya utekelezaji mpka sasa Bw.Gaspar Msigwa alisema  kuwa hadi sasa jumla ya wateja 1,652 wamekamilisha taratibu za malipo na tayari miundombinu ya umeme imekamilika kwa aslimia 90%.

    Msigwa ameongeza kuwa, licha ya juhudi hizo za serikali ya awamu ya tano, bado shirika linakabiliwa na changamoto ya wizi wa nyaya za umeme na baadhi ya watu kukosa uaminifu na kujiunganishia umeme bila kufuata taratibu. 

     Naye Loth Sabaya mkazi wa kata  Oljoro amesema kuwa  wamefurahishwa na nishati ya umeme kuwafikia kijijini kwao, na kuongeza kuwa kukosa umeme kunawacheleweshea maendeleo,na kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku za uzalishaji hasa zinazohitaji nishati ya umeme.

No comments