MADIWANI GEITA:Hatutishwi na Polisi
Madiwani wa Wilaya ya Geita wamesema hawatishwi na kamatakamata inayoendeshwa na jeshi la polisi ya kuwakamata madiwani walioshiriki kufunga barabara zinazoingia katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Baadhi ya madiwani wa wilaya Geita |
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Elisha Lupuga amesema kinachofanywa na polisi ni kuwatisha ili waache kudai fedha za Serikali jambo ambalo kamwe hawatakubali.
Amesema madiwani wameheshimu hekima ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga aliyewataka kuwa na hekima na busara na kusubiri uamuzi utakaotolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Merdad Kalemani Jumatatu wiki ijayo lakini wanashangazwa na kamatakamata inayofanywa na polisi.
“Tunasikia kwenye vyombo vya habari kamanda akisema madiwani wamekimbia hakuna anayekimbia kila mtu yupo kwenye kata yake na hata akitangaza kutuita tutaenda ofisini kwake au kituoni aache kutumia mafuta ya Serikali kuzunguka kutafuta madiwani atangaze tu kwamba anatuhitaji turipoti na sisi tutaripoti ili atukamate lakini hatutaacha kudai fedha zetu,”amesema Lupuga
Lupuga amesema madiwani wanaendelea na vikao vyao vya halmashauri na hakuna aliyekimbia na kumtaka Kamanda Mponjoli Mwabulambo kuacha kuwatisha wataendelea kudai mapato ya halmashauri hadi senti ya mwisho kwa sababu wao ni wawakilishi wa wananchi.
Amesema Septemba 18 watakua kwenye kikao katika ofisi ya mkuu wa mkoa kujadili hatma ya fedha hizo na kwamba ni wakati mwafaka polisi kuwakamata kwa sababu kudai mapato ya ndani ya halmashauri ni la kudumu hadi senti ya mwisho itakapolipwa.
Hadi sasa polisi mkoani Geita wanawashikilia madiwani wanane wa halmashauri za wilaya ya Geita waliofunga barabara zinazoingia mgodi wa GGM na kuharibu miundombinu ya maji yaliyotengenezwa na GGM kwa ajili ya shughuli za mgodi na wananchi wa mji wa Geita katika Kijiji cha Nungwe jambo ambalo ni kinyume na sheria
No comments