Header Ads

Serikali ya Kenya kumlipa mwanasiasa Sh945 milioni





Mwanasiasa mashuhuri nchini Kenneth Matiba, 85, aliyeteswa na vyombo vya dola katika miaka ya 1990 ameshinda kesi dhidi ya serikali na sasa atalipwa fidia ya shilingi za Kenya milioni 945.
Mwanasheria mkuu wa serikali Githu Muigai ameridhia kiasi hicho kipya kutoka Sh504 milioni alichopewa awali. Hii ni baada ya kugundulika kwamba kulikuwa na makosa katika ukokotoaji.
Mwezi uliopita, Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola alitoa hukumu iliyotaka serikali kumlipa Matiba fidia ya Sh504 milioni kwa mateso makubwa aliyopata akiwa katika mikono ya vyombo ya dola vya serikali.
Mwanasiasa huyo alikamatwa na polisi ambako alipata kiharusi Mei 26, 1991 lakini alibaki mahabusu kwa wiki moja bila kupewa dawa zozote. Katika kesi hiyo alitaka alipwe fidia ya Sh4,726,332,042.91, kwa kuteswa na kusababisha biashara yake kufa enzi za utawala wa Rais Daniel arap Moi.
Matiba ni miongoni mwa wanasiasa wanaharakati wa mageuzi ambaye alikamatwa na polisi, akawekwa kizuizini na hata ilipojulikana kwamba alikuwa ameugua kiharusi alibaki mahabusu bila dawa. Baada ya kutoka aliamua kutafuta haki yake mahakamani.
Hatimaye Agosti 16 ilisomwa hukumu. Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita akisoma hukumu kwa niaba ya Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenola alisema serikali inapaswa kulaumiwa kutokana na kuzorota kwa afya ya Matiba na kwa hiyo mahakama inaamuru alipwe Sh18 milioni kama fidia ya gharama za hospitali.
Pia, mahakama inaamuru Matiba ambaye aliwahi kuwa waziri alipwe na serikali Sh15 milioni kama fidi kwa mateso aliyopata. Kadhalika, mahakama iliamuru alipwe Sh471 milioni ikiwa ni fidia kwa biashara zake zilizokufa.
Hukumu hiyo ya Jaji Lenola ilisema, “Kitu kimoja cha uhakika moyoni mwangu; serikali iamuke na kuuelewa ukweli kwamba kwa sasa tabia za hovyo za zamani za maofisa wake na mawakala haziwezi kuachwa bila kuadhibiwa.
Matiba ataingia katika vitabu vya historia kuwa mrufani aliyelipwa kiasi cha juu cha fidia baada ya mahakama kuamuru hiyo kutokana na mateso.
Pamoja na kupewa tuzo hiyo kwa kesi aliyofungua, Matiba alisema anaendelea kuumia kisaikolojia na kwamba afya yake imeendelea kuzorota. Mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Kiharu alikosana na serikali Mei 1990 wakati yeye na mwenzake Charles Rubia walipoita waandishi wa habari kutoa wito wa kurejeshwa mfumo wa vyama vingi. Wawili hao walikamatwa na wakawekwa kizuizini bila kufikishwa kortini hadi mwaka 1991.
Matiba ambaye baadaye alianzisha chama cha Forum for the Restoration of Democracy (Ford), alikamatwa Mei 26 akawekwa kizuizini hadi Juni 4, 1991. Ukokotoaji ulipofanyika upya imebainika anastahili kulipwa Sh945 milioni na siyo Sh504 milioni.

No comments