Header Ads

SPIKA PIUS MSEKWA ANENA


Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa ametia neno akigusia utendaji wa Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyeingia katika msuguano na baadhi ya wabunge wa upinzani.

Ndugai ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma hakuwa na wakati mzuri katika Bunge lililomalizika jana kutokana na kupishana kauli na wabunge, Zitto Kabwe, Said Kubenea, Godbless Lema na Peter Msigwa.

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu Spika Ndugai alivyojikuta akitumbukia katika mvutano huo, Msekwa alisema: “tulifundishwa na Mzee Mwinyi(Ali Hassan) kila kitabu na zama zake.”

Amesema ingawa wakati wa uongozi wake hakukuwa na malumbano ya namna hiyo lakini hilo halimanishi kuwa Spika wa sasa anaendesha mambo kinyume na Kanuni za Bunge.

Amesema anachokifanya Spika Ndugai kinatafsiri aina ya uongozi alionao ambao siyo jambo la kushangaza kuona ukitofautiana na mfumo aliokuwa akitumia wakati akiwa katika kiti hicho.

“Hii ni staili yake ya uongozi na ndiyo mabadiliko ya uongozi wenyewe,” amesema Msekwa wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu na kurudia tena maneno hayo akisema “ ni staili yake na kila kiongozi anakuwa na mfumo wake wa kuongoza mambo.”

Lakini amesema kwa kufanya hivyo hajakosea lolote kwa vile yale aliyokuwa akiyazungumza na kuyatolea maamuzi yako ndani ya Kanuni za Bunge.
“Spika ametumia mamlaka yake sioni kama kuna ubaya wowote,” amesema Msekwa ambaye amewahi pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.

Amesema hata yeye alipochukua nafasi hiyo kulikuwa na maspika wengine waliomtangulia waliokuwa na mfumo wao wa kuendesha Bunge na kisha naye akawa na wake pia.
“Baada ya mimi walikuja wengine ambao nao pia walikuwa na staili yao ya uongozi,” amesema.

Hatua ya Ndugai kudai kuwa anaweza kumzuia Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe asizungumze bungeni kwa muda wote uliobaki na hana cha kumfanya imezusha mjadala mkubwa nchini huku baadhi ya wasomi wameikosoa kauli hiyo wakisema hana mamlaka hayo kisheria.
Spika Ndugai alitoa kauli hiyo hivi karibuni baada ya Zitto kunukuliwa katika akaunti yake ya Twitter akimkosoa kiutendaji.

Mzozo kati ya Spika Ndugai na Zitto ulianza baada ya kiongozi huyo wa ACT – Wazalendo kusema kwamba Bunge limewekwa mfukoni na mhimili fulani wakati alipotoa maoni kuhusu ripoti mbili za kamati ya Bunge za almasi na Tanzanite.

Kutokana na kauli hizo, Spika Ndugai aliagiza mbunge huyo ahojiwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku akimshtaki kwa wapigakura wake akisema licha ya kwamba mbunge wao yupo nchini hajafika bungeni kuwawakilisha na yeye (Spika), hana taarifa.

Wakizungumzia matamshi hayo baadhi ya wasomi walisema kauli kama hiyo haikupaswa kutolewa na Spika.
Baadhi ya wanasheria walisema kauli ya Spika Ndugai imelenga kuwanyamazisha wabunge wasiwe huru kutoa maoni yao kwa mujibu wa Katiba

No comments