Wanafunzi wanavyoisaka elimu kwa mitumbwi hatarishi Nkasi
Wakati baadhi ya wanafunzi nchini wakihitimu masomo yao bila changamoto za kielimu, kwa watoto wa Kisiwa cha Mandauhuru kilichopo wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa elimu hufuatwa kwa kupiga makasia ya mitumbwi kila siku za wiki kuvuka Ziwa Tanganyika.
Wanafunzi hao hulazimika kufanya safari hizo kwa kuwa katika kisiwa chao hakuna shule ya msingi ambayo ingewapunguzia safari ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita tatu kwenda kufuata huduma za elimu katika Kijiji cha Mkinga kilichopo nchikavu.
Kisiwa cha Mandauhuru ni miongoni mwa vijiji vitano vilivyopo katika Kata ya Mkinga kikiwa pamoja na Kalungu, Mkinga, Majengo mapya na Ntanganyika.
Baadhi ya wanafunzi waliliambia gazeti hili kuwa safari hizo zimekuwa ni sehemu ya maisha yao kwa sababu kijiji chao hakina shule wala zahanati.
Angela Michael anayesoma darasa la pili katika shule hiyo anasema yeye na wenzake wameshazoea kupiga makasia mitumbwi waliyotengenezewa na wazazi wao ili iwarahisishie usafiri wa kwenda na kurudi shuleni.
“Ni lazima kila siku tuamke asubuhi kisha tunakwenda ziwani ambako tunahifadhi mitumbwi yetu kisha tunakwenda shule. Tukimaliza masomo saa nane mchana tunarudi tena ziwani kuchukua mitumbwi yetu na kurudi nyumbani,” anasema Angela huku akitabasamu.
Wakiwa wanatoka shule, nilishuhudia wengi wao wakifika ziwani hapo na kuchukua makasia yao na kuivuta mitumbwi ambayo walikuwa wameiegesha pembezoni mwa ziwa.
Wenye mitumbwi waliwapa lifti wenzao wasiokuwa nayo na kisha kuanza kupiga makasia umbali wa kilometa mbili hivi hadi wafike kisiwani hapo huku mmoja wao, Michael John (9) akinikaribisha nisafiri nao.
John anayesoma darasa la kwanza anasema wazazi wao hawana uwezo wa kuwanunulia mtumbwi unaotumia injini hivyo wanalazimika kutumia mtumbwi wa kienyeji ili kwenda shule.
“Hatupewi hela nyumbani, kwa hiyo lazima tuje na kurudi kwa mitumbwi hii na tumeshazoea kuiendesha. Maji hanaya shida, kama ikitokea siku upepo ukipiga sana tunasubiri kwanza upite,” anasema John.
Sehemu kubwa ya wanafunzi hao ili wafike katika maeneo walipoiegesha mitumbwi yao wanalazimika kutembea kwa zaidi ya nusu kilomita kutoka makwao na ziwani hutumia takriban nusu saa iwapo ziwa litakuwa tulivu.
Pia, hulazimika kutembea takriban dakika 15 nyingine kufika shuleni baada ya kufika ng’ambo ilipo shule yao.
Kuna wakati kama hali ya ziwa inakuwa mbaya wanalazimika kuchelewa shule na hivyo hupitwa na baadhi ya vipindi.
“Muda wa kusafiri kwenye maji unategemea hali ya hewa, kuna wakati ziwa likichafuka inatubidi kusubiri litulie ndipo tuvuke, kwa hiyo tunajikuta tunachelewa shule,” anasema Angela.
Msongamano darasani
Hata pamoja na safari yote hiyo, wanafunzi hao wanakumbana na masaibu ya kujazana katika madarasa machache waliyonayo huku darasa la kwanza wakilazimika kusomea wanafunzi 200 kwenye chumba kimoja.
Shule hiyo ya Msingi ya Mkinga yenye wanafunzi 1,522 inahudumia vijiji vyote vitano vya Kata ya Mkinga.
Mwalimu wa shule hiyo, Bahati Mgaya anakiri kuwa wanafunzi wanakabiliwa na changamoto ya usafiri na kuongeza kuwa kuna ajali zilishawahi kutokea miaka ya nyuma, lakini wanafunzi waliokolewa.
“Kuna wanafunzi zaidi ya 90 wanaotokea katika hicho kisiwa, wameshazoea kuja na kurudi kwa mitumbwi. Zimewahi kutokea ajali tatu mwaka juzi lakini mara nyingi wanaogelea na kuokolewa,” anasema Mwalimu Mgaya.
Mwalimu Mgaya anasema wingi wa wanafunzi unawawia vigumu kuwafundisha kwa sababu ana walimu 13 tu ili hali walitakiwa walau wawepo walimu 33.
Uhaba wa walimu unafanya mwalimu mmoja katika shule hiyo afundishe wastani wa watoto 117 kinyume na kiwango kinachopendekezwa na Serikali cha mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40 wa shule za msingi na sekondari.
“Hapa tuko walimu 13 tu, wanaume tisa na wanawake wanne. Kwa utaratibu angalau mwalimu mmoja anatakiwa kufundisha wanafunzi 45 darasani ili awafikie vizuri. Kwa idadi hiyo ilitakiwa madarasa saba yawe na mikondo 35,” anasema na kuongeza:
“Lakini hapa darasa la kwanza pekee yake lina wanafunzi 636, imebidi tuligawe katika mikondo mitatu, kwa hiyo mwalimu anafundisha wanafunzi zaidi ya 200. Unajua mwaka huu kumekuwa na mwamko mkubwa wa kuandikisha watoto shule.”
Anasema kwa sasa imekuwa vigumu kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu kwa sababu ni tatizo la wilaya nzima ya Nkasi.
“Unajua Serikali haijaajiri walimu kwa miaka miwili sasa, nimeshawaambia wilayani wamesema nisubiri ajira mpya. Awali walisema watahamishia walimu kutoka kwenye shule zenye walimu wengi, lakini hili ni tatizo la wilaya nzima.
“Kwa mfano kuna shule inaitwa Isunda yenye wanafunzi zaidi ya 2,000 na walimu 32 tu, sasa utawahamishaje hao walimu? Kwa suluhisho ni ajira mpya tu,” anasema.
Kuhusu uhaba wa vyumba vya madarasa, mwalimu huyo anasema kwa sasa wanakabiliana na changamoto hiyo kwa wananchi kujenga kwa kujitolea kulingana na agizo la mkuu wa wilaya hiyo.
Hata hivyo, Mwalimu Mgaya anasema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba ambapo mwaka 2016 wanafunzi 64 kati ya 79 walifaulu na kujiunga kidato cha kwanza.
Mwenyekiti wake, Venance Kapunda anasema ndiyo kwanza kimepewa hadhi ya kuwa kijiji mwaka 2015 na juhudi za ujenzi wa shule zimeanza.
“Ni kweli wanafunzi wanakwenda kusoma Shule ya Msingi Mkinga kwa kuvuka maji. Tumepewa hadhi ya kuwa kijiji mwaka 2015, tuko kwenye ujenzi wa shule kwa kuanza na madarasa mawili,” anasema Kapunda.
Akizungumzia changamoto ya watoto kusafiri kwa kutumia mitumbwi ya kienyeji, Kapunda anasema mwaka 2013 watoto sita walizama ziwani baada ya mtumbwi kupigwa na mawimbi lakini wazamiaji wawaahi na kuwaokoa.
Anasema kwa kutambua changamoto hiyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy alitoa mtumbwi wa injini ambao pia hutumiwa kwa dharura kama hizo.
“Hiyo ni changamoto kubwa kwa usalama wa watoto wetu, lakini hatuna budi kuhakikisha wanapata elimu. Ndiyo maana tumeanza ujenzi wa shule ili wasiendelee kwenda Kijiji cha Mkinga,” alisema Kapunda.
Mbali na wanafunzi wanaotoka Kijiji cha Mandauhuru, kuna visiwa vingine kama Mvuna ambacho hakina shule pia na kiko mbali na nchi kavu hali inayosababisha zaidi ya watoto 200 kushindwa kwenda shule kabisa.
Vilevile katika Kisiwa cha Mandakerenge, licha ya kuwa na shule baadhi ya wanafunzi wanatembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa 10 kwenda na kurudi shule kila siku. Kisiwa hicho kina vitongoji 13 vyote vikitegemea shule moja ya Msingi ya Mandakerenge.
Hata hivyo, diwani wa Kata ya Mkinga, Reuben Kisi anaonyesha kuwa hakuna dalili za kuboreshewa usafiri kwa sasa akisema mpango uliopo ni kujenga tu madarasa manne kwa ajili ya darasa la kwanza na la pili katika Kijiji cha Mandauhuru kisha wanafunzi wengine wataendelea kusafiri kwa mitumbwi kwenda Shule ya Msingi Mkinga.
“Pale Mandauhuru tulishaona haina jinsi, nilizungumza na wanakijiji tukakubaliana kujenga madarasa manne kwa ajili ya watoto wadogo, wakishapata akili ndiyo waendelee kuvuka maji kuja Shule ya Msingi Mkinga. Haina jinsi,” anasisitiza Kisi.
Kauli ya mbunge
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy amekiri kuwepo changamoto ya usafiri na huduma nyinginezo katika visiwa hivyo huku akibainisha kuwa ameshatoa mtumbwi wa injini kwa ajili ya kusaidia wananchi katika Kisiwa cha Mandauhuru.
Hata hivyo, Keissy aliyezungumza kwa njia ya simu, anasema Kisiwa cha Mandauhuru pamoja na kata nzima ya Mkinga ina watu wachache hivyo huduma zilizopo zinatosha.
“Wakazi wa Kisiwa cha Mandauhuru hawafiki hata watu 200 utapelekaje huduma za jamii pale? Tutakachofanya ni kujenga tu madarasa manne yanayowatosha. Mimi ndiyo mbunge ninaelewa hiyo kero,” anasema Keissy.
Serikali inasema matatizo ya huduma za kijamii yaliyopo katika visiwa hivyo ni ya kihistoria kwa kuwa Mkoa wa Rukwa ulikuwa nyuma kimaendeleo kwa muda mrefu.
Wadau wa elimu wanaishauri Serikali kuhakikisha mazingira ya kujifunzia yanakuwa sawa kwa watoto wote ili wapate haki ya kupata elimu.
No comments