Jinsi tukio la Lissu lilivyomuibua Nyalandu
Dar es Salaam. Amewahi kufanya, amefanya na sasa anafanya juhudi za kusaidia watu waliopatwa na majanga.
Lakini safari hii, mtazamo kwa anayoyafanya ni tofauti.
Ndivyo ilivyo kwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu, ambaye jitihada zake za kumjulia hali na kuhimiza maombi kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliyejeruhiwa kwa risasi Septemba 7, sasa zinaangaliwa kwa jicho tofauti.
Nyalandu alishiriki kuwajulia hali majeruhi wa mlipuko wa bomu kanisani wakati wa uzinduzi wa Parokia ya Olasiti, Jimbo Kuu la Arusha na akawa waziri pekee aliyejitolea kutafuta ndege ya kuwapeleka Nairobi nchini Kenya kw amatibabu zaidi, wakati huo akiwa naibu waziri wa Maliasili na Utalii.
Pia alishiriki kikamilifu, akishirikiana na taasisi ya Elimu ya Afya ya Sioux na Tanzania (Stemm) kutafuta msaada wa usafiri wa kwenda Marekani na matibabu kwa watoto watatu wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent walionusurika katika ajali ya basi dogo iliyoua wanafunzi 29, walimu wawili na dereva.
Wanafunzi hao Doren Mshana, Wilson Tarimo na Sadya Awadh wamesharejea nchini wakiwa katika hali nzuri baada ya ajali hiyo kuwaacha katika hali mbaya na wamesharejea shuleni.
Hivi sasa, mbunge huyo anaonekana kuwa katika harakati za kumtakia afya njema na kumuombea Lissu, ambaye alishambuliwa kwa takriban risasi 32 nje ya majengo ya makazi yake mjini Dodoma, tukio ambalo Nyalandu amelielezea akiwa mjini Mbeya kuwa “ni la kisiasa”.
Kupigwa risasi kwa Lissu, ambaye alikuwa Dodoma kutekeleza majukumu yake ya kibunge, kuliwaibua wabunge walioliomba Bunge kuunda timu ya kwenda jijini Nairobi kumjulia hali mwenzao, lakini kiti cha spika kilikataa hoja hiyo kwa maelezo kuwa tayari baadhi yao walishaenda kuwawakilisha.
Wabunge ambao wakati huo walikuwa Nairobi ni Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema na mbunge wa Hai, na Mchjungaji Peter Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini wa chama hicho.
Wakati wabunge wakilalamika kukosa ruhusa ya Bunge, kulikuwa na malumbano kuhusu ushiriki duni wa Serikali na Bunge katika kumuuguza Lissu aliyepigwa risasi katika kipindi ambacho alishatoa malalamiko kuwa kulikuwa na watu asiowafahamu waliokuwa wanamfuatilia.
Lakini, Nyalandu alijitokeza na kwenda Nairobi kumuona Lissu, akiandika katika akaunti zake za mitandao ya kijamii kuhusu safari hiyo na maendeeleo ya ziara yake, huku akituma picha zinazomuonyesha akiwa hospitalini.
Mbali na kumjulia hali na kuhimiza wananchi wamuombee, harakati za Nyalandu zimekuwa zikiambatana na ujumbe unaonekana kuwa na utata, ambao umemfanya atafsiriwe tofauti, akihimiza wananchi upendo, amani, kuvumiliana na haki kushinda dhuluma.
Pia, Nyalandu, ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka 2000, amelielezea tukio la kushambuliwa kwa Lissu kuwa ni kurudi nyuma kidemokrasia huku akiwaita waliomshambulia kuwa ni waonevu na kutaka Serikali ifanye jitihada kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki.
“Sote tuungane katika kufanya maombi maalumu kwa ajili ya #TunduLissu, na kwa wale walio karibu na mji wa Mbeya, naomba muungane nami katika Kanisa la Ebenezer,” ameandika Nyalandu katika ukurasa wake wa Facebook.
Katika video aliyotuma kwenye ukurasa huo, Nyalandu anasema: “Nimekuja Mbeya kulikumbusha Taifa kuwa kupigwa kwa mmoja wetu ni kupigwa kwetu sote, kuumizwa kwake ni kuumizwa kwetu sote, na kudhulumiwa kwake huyo mmoja ni dhuluma dhidi ya kila Mtanzania.
“Tundu Lissu amepona kwa kuwa imeandikwa (katiba Biblia) ‘hatasinzia yeye akulindaye’, na kwetu kama Taifa, tukasimama naye wakati huu wa kujaribiwa kwake. Naamini ndani ya moyo wake akiwa katika maumivu lukuki aliyonayo, #TunduLissu atakuwa anajiuliza nimekukosea nini Taifa.”
Wakati katika baadhi ya maeneo, watu walizuiwa kukusanyika kufanya maombi kwa ajili ya mwanasiasa huyo, Nyalandu anahimiza katika ujumbe wake kuwa Lissu aombewe “kimya, na tumwombee kwa sauti, tuombe mahali pa sirini, na tuombe hadharani”, akisema kuwa wameagizwa “kulia na wanaolia, kwenda kuwaona wagonjwa na waliofungwa, na tuwatangazie kufunguliwa kwao”.
“Naaam, hii ndiyo siasa sahihi ya utu kabla ya itikadi, upendo kabla ya visasi; heshima kabla ya husuda,” anasema Nyalandu.
“Watanzania wote tusimame, miguu yetu ikatiwe utayari, roho ya mapenzi na ujasiri ikatamalaki na kuondoa roho ya hofu na ganzi (spirit of indifference), tukaipandishe tena bendera yetu pale kileleni Kilimanjaro.
“Yamkini kwamba haki iishinde dhuluma; umoja wetu, ushinde roho ya matengano; na sauti za walioteswa na kuonewa zisikike na kuleta tena tumaini jipya la amani, haki, upendo, na mshikamano.”
Wiki mbili zilizopita, mchangiaji mmoja katika mitandao ya kijamii alielezea harakati hizo za Nyaloandu kuwa ni kujiandaa kugombea ubunge wa Arusha Mjini, akigusia kuwa ni mpango wa chama kimoja cha kisiasa.
Wasemavyo CCM
Lakini watu walioongea na Mwananchi walikuwa na mawazo tofauti, ingawa viongozi wa chama chake walionyesha kusita.
Wakati katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga akimtaka mwandishi wetu amtafute Hamphrey Polepole azungumzie suala hilo, katibu huyo wa itakadi na uenezi alimtaka mwandishi amtafute Nyalandu na kumuuliza kama anaelekezwa na CCM au anafanya hivyo kwa upendo wake binafsi.
Hata hivyo, Kanali Lubinga alieleza kuwa Watanzania wanaishi kama ndugu na kwamba, mtu akiwa chama fulani haimanishi kama ana ugomvi na mtu mwenye chama tofauti na chake.
“Haimaniishi mtu akiwa CUF na wewe upo CCM ndiyo mnakuwa na ugomvi. Si hivyo watu tunaishi kama ndugu,” alisema Kanali Lubinga.
Lakini mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen-Kijo Bisimba alisema Nyalandu anaonekana tofauti kwa wana-CCM wenzake, licha ya kuwa na moyo wa kujitolea na anafanya hivyo kwa Lissu kwa kuwa wanatoka mkoa mmoja.
“Nyalandu hayupo ndani ya Serikali na hapa inawezakana akawa anawakilisha kundi kubwa la watu wa Serikali na chama chake ambao wanataka kumsaidia Lissu kwa njia yoyote; iwe maombi au la, lakini wanaogopa kutoka hadharani,” alisema Dk Bisimba.
Dk Bisimba alitoa mfano wa baadhi ya wabunge wa CCM waliokwenda kumuona Lema aliyekuwa gereza la Kisongo mkoani Arusha baada ya kunyimwa dhamana.
“Wabunge hawa wanajua kilichowakuta kwa sababu walisemwa sana na chama chao na baadhi yao ilifika hatua walijiuzulu nyadhifa zao katika kamati za kudumu za Bunge walizokuwa wakiongoza,” alisema Dk Bisimba
Naye mkurungezi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa alisema kinachofanywa na Nyalandu ni sahihi na ndiyo siasa zinazotakiwa kwa sababu hajali itakadi za vyama katika matatizo.
Alitoa mfano wa jinsi alivyojitolea kusaidia watoto wa Lucky Vincentambao wanatoka Arusha ambako upinzani umeshamiri.
Ole Ngurumwa alisema ni wakati mwafaka kwa chama chake kujitokeza hadharani na kumuunga mkono kwa kuwa ni mfano wa kuigwa
No comments