Header Ads

jaji Maranga atikisa Dar es Salaam









Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga jana aligeuka kivutio wakati wa mkutano wa siku tatu wa majaji na mahakimu kutoka nchi za Jumuiya ya Madola (CMJA) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazowakabili.
Maraga, ambaye jopo lake lilifuta uchaguzi wa Rais wa Kenya na kuamuru urudiwe, alishangiliwa baada ya kutambulishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, jambo ambalo halikufanyika kwa majaji wakuu wa nchi nyingine.
Mwanasheria huyo nguli wa Kenya alikuwa ameambatana na watu wanne wanaonekana kuwa walinzi wake na ambao walimfuata kila alipokwenda nje ya ukumbi wa mkutano wa Benki Kuu (BoT), akiwa anaongea na watu ambao baadhi walitaka kupiga naye picha.
Hata hivyo, Maraga hakutaka kuzungumza chochote na vyombo vya habari kwa maelezo kuwa amekuja kuhudhuria mkutano tu.
Katika hotuba yake, Profesa Juma alisema Maraga ameacha alama kubwa.
“Nalazimika kumtaja kipekee Jaji Mkuu wa Kenya David Kenani Maraga ambaye pia amehudhuria mkutano huu,” alisema Profesa Juma.
“Hii ni baada ya kutumia zaidi ya saa kumi na moja Jumatano ya Septemba 20, 2017 kutoa uamuzi wa wengi na wachache wa Mahakama Kuu ya Kenya ulioacha alama.
“Tunajisikia kupewa heshima ya dhati kwa uwepo wako Mheshimiwa, Jaji Mkuu Maraga.”

Jaji mku wa Kenya David Maraga
Akifungua mkutano huo unaohudhuriwa na majaji wakuu wa nchi 13, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alisema rushwa ni kitu kinachoondoa uhuru wa mahakama na utawala wa sheria.
Samia alisema Tanzania inapambana na rushwa ili kuhakikisha mahakama inatoa haki kwa wakati na kwa viwango.
Alisema majaji na mahakimu wana wajibu wa kuhakikisha mahakama inakuwa huru kwa kuzingatia maadili.
Kiongozi huyo alisema changamoto kubwa inayozikabili nchi mbalimbali duniani ni uhaba wa fedha, jambo ambalo linaathiri mifumo ya utoaji haki na hivyo Serikali inajitahidi kuongeza bajeti ya mahakama kila mwaka.
Kwa upande wake, Profesa Juma alisema bajeti ya Mahakama imeongezeka kwa asilimia 100 na wameanza kutekeleza mipango mbalimbali ya kuboresha utendaji.
Profesa Juma alisema katika mpango wa miaka mitano, watajenga mahakama 48 za wilaya, 100 za mwanzo na majengo 13 ya Mahakama Kuu 13.
“Bajeti inayokidhi mahitaji ni muhimu sana kwa uhuru wa mahakama,” alisema.

No comments