Ajali ya lori yaua watu 15 Sumbawanga.......Rai Magufuli Atuma Salamu za Rambi rambi
Sumbawanga. Watu 15 wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa baada ya lori walilokuwa wakisafiria kupinduka eneo la Ntembwa ndani ya Hifadhi ya Lwafi wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Ajali hiyo imetokea jana Jumanne saa mbili usiku baada ya lori aina ya Fuso lililokuwa likitoka Kijiji cha Mvimwa kuelekea Kijiji cha Wampembe kupinduka. Lori hilo lilikuwa limebeba mahindi na abiria.
Kutokana na ajali hiyo, Rais John Magufuli amemtumia rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Stephen, familia za marehemu, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na vifo hivyo.
Katika taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli amewaombea majeruhi wa ajali hii wapone haraka ili warejee katika afya njema na kuungana na familia zao katika maisha yao ya kila siku.
Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama barabarani kuongeza juhudi zitakazowezesha kukabiliana na matukio ya ajali ili kuokoa maisha ya watu na mali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando katika taarifa amesema lori hilo liligonga mwamba kabla ya kupinduka.
Kyando amesema watu 12 walikufa papo hapo na wengine watatu walifariki baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa. Amesema dereva wa lori hilo alikimbia baada ya ajali kutokea.
No comments