JPM sitakubali mwenge ufutwe kama wana siasa wengine wanavyo taka
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amesema kuwa katika kipindi chake cha uongozi, Mwenge wa Uhuru utaendelea kukimbizwa nchi nzima kila mwaka, na kwamba hatokubali ufutwe kama ambavyo baadhi ya wanasiasa na wananchi wengine wamekuwa wakishinikiza.
Akizungumza akiwa Mkoa wa Mjini Magharibi mjini Zanzibar katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Miaka 18 ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana, Rais Magufuli amesema siyo yeye tu, kwani hata Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Shein watakaokubali kufutwa kwa mwenge huo.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo mashinikzo kutoka kwa watu mbalimbali nchini wakitaka mwenge wa uhuru ufutwe kwa madai kuwa umekuwa ukiigharimu serikali kiasi kikubwa cha fedha katika kipindi chote cha miezi 6 ambacho huwa unakimbizwa nchi nzima.
Akiyasema hayo, Rais Magufuli alitoa sababu tatu, kwanini katika kipindi chake mwenge hautofutwa ambapo, moja ya sababu ni kuwa, mwenge huo unachochea maendeleo ya nchi.
Rais Magufuli amesema wale wanaosema kuwa mwenge unatumia fedha nyingi hawajui namna unavyoendeshwa kwani mwenge unapopita katika kila halmashauri, huwa wanahakikisha wanamradi mpya ambao utazinduliwa mwenge utakapofika, na hii huwalazimu kujituma zaidi katika kujenga miradi.
Lakini Rais alieleza kwamba, mwaka 2017 serikali ilitenga Tsh 460 milioni kwa ajili ya mbio za mwenge, lakini umezindua miradi ya mabilioni pamoja na kubaini miradi mingine ambayo ni mibovu na kuamuru wahusika kuchukuliwa hatua. Rais amesisitiza kwamba, kama mbio za mwenge zisingefanyika, huenda viongozi wa vijiji wasingejituma kufanikisha miradi hiyo, na hata hiyo mibovu isingebainika.
Sababu ya pili ya kutokufutwa kwa mwenge huo, Rais alisema kwamba unaunganisha watanzania. Akitolea ufafanuzi suala hili, Rais Magufuli amesema kwamba, kwanza mwenge hukimbizwa katika pande zote za muungano, lakini pia watu wanaoukimbiza hutoka pande zote.
Jambo hili ni muhimu sana kwa sababu linadumisha muungano wetu, kuimarisha ushirikiano pamoja na kudumisha udugu baina ya pande mbili za muungano.
Jambo la tatu ambalo Rais amesema ni sababu kwake kutofuta mwenge wa uhuru, alisema, mwenge huo ni alama ya uhuru wa taifa ambao kwa mara ya kwanza uliwashwa Disemba 9 mwaka 1961 wakati Tanzania (Tanganyika wakati huo) ilipopata uhuru.
Katika hotuba hiyo, Rais alieleza kuwa, kwenye mbio za mwenge 2017, viwanda 148 vyenye thamani ya Tsh 468bn vitakavyotoa ajira 13,370 vimezinduliwa nchi nzima.
Pia alisema anawashangaa wanaotaka mwenge huo ufutwe, kwani wao ndio huwa mstari wa mbele kupokea Kifimbo cha Malkia au kushiriki kwenye mwenge wa Olimpiki.
No comments