Header Ads

Miaka 18 Hayati Mwalimu Nyerere Atakumbukwa Kwa Juhudi Za Kuimairisha Sekta Ya Utalii Nchini


Image result for nyerere
“Uhai wa wanyamapori ni jambo linalotuhusu sisi sote katika Afrika, viumbe hai wa porini wakiwa katika mapori waishimo sio muhimu tu kwa ajili ya kuajabiwa na kuvutia lakini pia ni sehemu ya maliasili yetu na mustakabali wa maisha yetu baadaye”

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema hayo wakati akitoa tamko la Arusha kuhusu Uhifadhi wa wanyamapori kipindi Tanganyika inapata Uhuru mwaka 1961.

Alisema kukubali dhamana ya wanyamapori, watanzania wanawajibu wa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wajukuu na watoto wa kitanzania wanaweza kufurahia urithi mkubwa wa thamani hiyo adhimu ya wanyamapori.

Juhudi za uhifadhi na kulinda rasilimali, malikale na kuendeleza shughuli za ufugaji nyuki pamoja na kukuza Sekta ya Utalii ikiwa ni jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii zilikuwepo hata kabla ya ukoloni ambapo jamii nchini zilitenga mapori kwa ajili ya kuabudia na kutambika.

Kuingia kwa wakoloni nchini kuliambatana na kutunga Sheria za uhifadhi wa rasilimali za maliasili na malikale ambapo ni Sheria ya kuhifadhi Majengo ya kihistoria ya mwaka 1937, Sheria ya Makumbusho ya mwaka 1941, Sheria ya Usimamizi wa Misitu ya mwaka 1957, Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ya mwaka 1959, Sheria ya Hifadhi za Taifa ya mwaka 1959 na Sheria ya kuhifadhi wanyama ya mwaka 1959.

Chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kuanzia mwaka 1961 Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa na Sera na Sheria tofauti kulingana na mabadiliko yaliyokuwa yakitokea duniani katika nyanja za kiuchumi, kiteknolojia, kiasiasa na kijamii.

Juhudi za Baba wa Taifa katika kuhakikisha Sekta ya utalii mwaka 1961 ilikuwa na idara moja ambapo ilianza kuwa na Sera ya uhifadhi wa maliasili, malikale na kuendeleza utalii nchini.

Mabadiliko na matukio makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii mara baada ya uhuru mwaka 1961 yalipelekea jitihada za makusudi za kuwezesha wazawa kielimu ili kuweza kuchukua nafasi za utendaji na uongozi ambazo awali zilishikiliwa na wageni.

Aidha, mwaka 1967 kufuatia kupitishwa Azimio la Arusha mali binafsi zilitaifisha na kuundwa kwa mashirika na taasisi za umma ambapo Wizara iliunda mashirika ya umma ikiwemo Shirika la Wanyamapori, Shirika la Viwanda vya mbao, Shirika la Utalii Tanzania, Shirika la kuhudumia wasafiri na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kukuza na kuimarisha sekta ya utalii nchini.

Katika mabadiliko hayo ndani ya Wizara, juhudi za Mwalimu Nyerere zilipelekea Serikali kujitoa katika kuendesha shughuli za kibiashara na kujikita katika kusimamia Sera na uwezeshaji.

Kadhalika katika suala la ulinzi wa rasilimali za maliasili za taifa, Serikali ilirithi mfumo wa kikoloni na kuendelea kuwa mlinzi na mwendelezaji mkuu wa rasilimali za maliasili, malikale na utalii.

Miaka 1991 Serikali ilifanyika mabadiliko ya kisera yaliyokuwa na mwelekeo wa uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali kwa kuhimiza ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali za maliasili, malikale na utalii.

Ushirikishwaji huu wa jamii katika shughuli za maliasili na utalii ulipelekea Wizara kuanzisha vitengo mbalimbali ikiwemo kitengo cha Ugani katika idara na taasisi zake ikiwa na lengo la kuimarisha na kukuza sekta ya utalii nchini.

Katika suala la ajira katika wizara wakati nchi inapata  uhuru, jinsia haikupewa kipaumbele katika sekta za maliasili hususani wanyamapori, misitu, malikale na nyuki. Kazi hizo zilikuwa maalumu kwa wanaume ambapo juhudi za Mwalimu Nyerere zilipekea mabadiliko ya kimtazamo uliosababisha kupatikana kwa ajira ikihusisha jinsia zote mbili, ambapo kwa mara ya kwanza sekta ya utalii iliajiri mwanamke mwaka 1970.

Katika sekta ya nyuki wanawake wawili waliokuwa na astashahada ya ufugaji wa nyuki waliajiriwa mwaka 1975, sekta ya misitu iliajiri mwanamke wa kwanza mwenye shahada mwaka 1976, katika sekta ya wanyamapori mwanamke aliajiriwa mwaka 1967 na katika sekta ya mambo ya kale mwanamke aliajiriwa mwaka 1978 kwa ngazi ya cheti na 1981 kwa ngazi ya shahada.

Katika kuongeza tija na kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa zilizofanyiwa utafiti, wizara ilianzisha vyuo vya ulinzi, uhifadhi na uendelezaji wa maliasili, malikale na utalii ambapo chuo cha viwanda vya misitu kilianzishwa mwaka 1975, chuo cha ufugaji nyuki Tabora mwaka 1978 pamoja na vyuo vya elimu ya wafanyakazi Rongai na Sao Hill vilivyoanzishwa mwaka 1979 kwa lengo la kutoa elimu ya awali ya uoteshaji miche na kuhudumia misitu.

Katika kukuza na kuimarisha sekta ya utalii nchini Mwalimu Nyerere aliweza kutekeleza majukumu ya wizara kulingana na mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea nchini na duniani katika nyanja ya kiuchumi, kisiasa kiteknolojia na kijamii.

Juhudi hizo zilipelekea wizara kuongeza vituo vya malikale na kutangaza maeneo tofauti kama urithi wa Taifa, mashamba ya miti yaliongezeka, misitu ya asili pamoja na hifadhi za Taifa kuongezeka.

Mbali na juhudi hizo za Mwalimu zilisaidia kukuza na kuimarisha sekta ya utalii mara baada ya uhuru zilipelekea ongezeko la mikusanyo ya malikale ambapo wakati wa uhuru wizara ilihifadhi jumla ya mikusanyo ya 10,151 ya fani za Akiolojia, mila, historia, bayolojia na nyaraka mbalimbali.

Aidha, baada ya uhuru kutokana na tafiti zilizofanywa na watafiti wazawa na wageni kutoka nje ya nchi hadi juni, 2011 wizara imefanikiwa kuhifadhi nchini urithi wa malikale unaohamasisha wenye jumla ya mikusanyo 337,361.

Katika suala la ongezeko la idadi ya watalii wanaongia nchini ndani ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 9,847 mwaka 1960 hadi watalii 103,361 mwaka 1986.

Tukiwa tunaadhimisha miaka 18 bila Mwalimu Nyerere kumekuwa na mafaniko makubwa katika sekta ya utalii ambapo mpaka kufikia mwaka 2016 idadi ya watalii waliotembelea nchini Tanzania ilifika 1,284,279

Ukuaji huo wa sekta ya utalii unatokana na misingi imara iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuendelezwa na kusimamiwa kwa manufaa ya sasa na baadaye.

No comments