Header Ads

DKT.SHIKA ATIKISA KAHAMA




Mkuu wa wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu leo amezidua rasmi chuo cha Sayansi ya afya kilichopo Mjini Kahama mkoani Shinyanga ambapo uzinduzi huo umeambatana na mahafali ya kwanza ya wahitimu wa mafunzo hayo katika chuo hicho. Uzinduzi huo umehudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya wilaya ya Kahama akiwemo Mtanzania aliyejizolea umaarufu hivi karibuni Dr. Louis Shika ambaye ameahidi kutoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kusomesha wanachuo ambao wazazi wao wameshindwa kuwalipia ada na wale ambao ni yatima wazazi wao wamefariki dunia.


Akizungumza katika hahafali hayo yaliyofanyika leo Alhamis Novemba 23,2017 Nkurlu aliwataka wahitimu wa fani mbalimbali wilayani Kahama kuwa waadilifu pale wanapopata nafasi ya kuihudumia jamii ili kukidhi matakwa ya kusomea fani hizo.
Nkurulu alisema baadhi ya wahitimu wa mafunzo mbali mbali wamekuwa wakishindwa kukidhi vigezo kutokana na kutokuwa na nia ya dhati ya kutekeleza wajibu wao kwa weledi na uadilifu.
Katika hatua nyingine Nkurlu alimwelezea Dr. Shika kuwa ni mtu wa pekee mwenye utulivu na usikivu na kuongeza kuwa wadau wengine waige kama alichofanya Dr. Shika katika kuinua elimu nchini.
Kivutio kikuu katika sherehe hizo akawa Dr. Louis Shika ambaye hivi karibuni amejingea umaarufu, alipojitokeza katika mnada wa nyumba za kifahari za Bilionea Saidi Lugumi zilizoko jijini Dar es salaam, kupitia msemo wake wa “(900 INAPENDEZA)” ambapo katika mahafali hayo ameahidi kutoa bilioni mbili kila mwaka kusomesha watoto yatima katika wilaya ya Kahama.
Dr. Shika alisema kuwa yeye ni mpenzi wa elimu na anapenda watu wote wapate elimu hivyo kupitia kampuni yake ya Lancefort atasaidia kusomesha wanachuo ambao wazazi wao wameshindwa kuwalipia ada na wale ambao ni yatima wazazi wao wamefariki.
Ahadi hiyo imekuja kufuatia risala ya chuo hicho iliyosomwa na Mkuu wa Chuo hicho na kuelezea changamoto wanazokutana nazo kuwa ni pamoja na wazazi kushindwa kulipa ada pamoja na waanachuo wengine kushindwa kuhitimu mafunzo yao baada ya wazazi wao kufariki.
Dr. Shika alitoa wito kwa ofisi ya mkuu wa wilaya imuombe kusaidia kusomesha wanafunzi wasio na uwezo kwani kampuni yake inauwezo wa kusaidia watoto yatima katika wilaya ya Kahama hivyo milango iko wazi na yeye yuko tayari kusaidia watu wenye njaa ya elimu.
Akielezea kiwango atakachokitoa kusomesha wanachuo hao, Dr Shika amesema kuwa itakuwa ni dola milioni moja za Kimarekani sawa na Bilioni mbili ambazo atakuwa anazitoa kila mwaka kwa chuo hicho kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaopenda kusoma lakini wanashindwa kutokana na ukosefu wa ada.
Katika hatua nyingine Dr Shika aliwataka waandishi wa habari na mwenye chuo wasimuulize kuhusu msaada huo ndani ya wiki mbili kwani kwasasa hana pesa bali wasubiri mpaka mchakato wake wa kuhamisha fedha zake kutoka Urusi ukamilike.
Naye mkurugenzi wa chuo hicho Yonah Bakungile amesema kuwa kumekuwa na shida ya wanafunzi wanaomaliza vyuo vya uuguzi kutokuwa na maadili na kufikilia masirahi jambo ambalo limechangia kupoteza maana halisi ya masomo hayo.
Aliwataka kuitumikia jamii bila kuangalia maslahi na kuwahudumia watu walio nacho na wasiokuwa nacho ikiwa ni kutimiza malengo na nia ya kuanzisha vyuo vya uuguzi katika kuihudumia jamii katika maeneo mbali hapa nchini.

Aidha alisema baadhi ya Wahitimu wa vyuo vya uuguzi wanakosa uadilifu na kuweka mbele maslahi binafsi hulka inayopoteza maana halisi ya fani hiyo.
Amewataka kuitumikia jamii bila ubaguzi na kuangalia maslahi binafsi ili kwenda sanjari na matakwa na viapo vya kada ya uuguzi duniani.
Katika Mahafali hayo ya kwanza, Jumla ya Wahitimu 33 wametunukiwa cheti cha Msingi katika Kozi ya Mwaka mmoja ya Ufamasia.
Chuo cha Sayansi ya Afya Kahama kilianzishwa mwaka 2016 kikitoa mafunzo katika fani za Ufamasia na Utabibu na kwamba jumla ya wanachuo 33 wamehitimu.

No comments