Header Ads

Magufuli na Museveni waahidi kuimarisha ushirikiano

Magufuli na Museveni Alhamisi waliweka jiwe la msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki katika kijiji cha Luzinga, Mutukula nchini Uganda.
Magufuli na Museveni Alhamisi waliweka jiwe la msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki katika kijiji cha Luzinga, Mutukula nchini Uganda.

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na mwenzake wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wameahidi kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao mbili.
Wawili hao wamewaagiza Mawaziri wa nchi hizi mbili kujadiliana juu ya namna ya kuongeza biashara kati ya nchi hizo ili kupata manufaa makubwa zaidi ya uhusiano na ushirikiano uliopo.
Dkt Magufuli na Bw Museveni walitoa agizo hilo baada ya kufanya mazungumzo rasmi katika Ikulu ndogo ya Masaka nchini Uganda ambako Rais Magufuli ameendelea na ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku tatu.
Rais Magufuli amesema kwa muda mrefu biashara kati ya Tanzania na Uganda imekuwa ni takribani shilingi Bilioni 200 kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo mno ikilinganishwa na fursa zilizopo, uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliojengwa tangu enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
"Tumewaagiza Mawaziri na wataalamu wakae na waangalie vikwazo vyote vinavyosababisha tufanye biashara kwa kiasi kidogo, wakishajadili watatuambia tufanye nini, tunataka kuona biashara ya Tanzania na Uganda inakua," alisema.
"Hivi sasa Uganda imewekeza Dola za Marekani Milioni 47 tu nchini Tanzania na kuzalisha ajira 146,000, kiasi hiki ni kidogo sana, ni lazima tuongeze."
Tanzania, Dkt Magufuli alisema, pamoja na kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726, imekarabati reli iliyopo, pamoja na kivuko cha mabehewa ya treni cha Umoja katika Ziwa Victoria ili kuwezesha mizigo ya kutoka bandari ya Dar es Salaam kufika Kampala kwa gharama nafuu na pia inaendelea kujenga na kuimarisha barabara za mpakani.
Uganda nayo itajenga kipande cha kilometa 11 za reli kutoka Portbell hadi Kampala.
"Na sisi tumeamua kuweka bandari kavu pale Mwanza ili wafanyabiashara wa Uganda wasisumbuke kwenda hadi Dar es Salaam, mizigo yao wataipata Mwanza, hii ni njia ya uhakika na nafuu ya kusafirisha mizigo," alisema Dkt Magufuli.
Dkt Magufuli akiwa katika makazi ya Rais wa Uganda yaliyopo Masaka-Uganda
Dkt Magufuli akiwa katika makazi ya Rais wa Uganda yaliyopo Masaka-Uganda
Rais Museveni amesisitiza kukuzwa kwa biashara katika ya Tanzania na Uganda hasa wakati huu ambapo alisemaUganda inahitaji kununua gesi ya Tanzania kwa ajili ya viwanda vyake vya mbolea na chuma na pia kurudisha historia ambapo Uganda ilikuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa za Tanzania.
Marais wote wawili walishuhudua utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji wa Uganda (UBC) na makubaliano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Jeshi la Polisi la Uganda.

No comments