Header Ads

Mbunge Nape Nnauye akosoa miradi ya serikali


Mbunge wa Mtama kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amekosoa utekelezaji wa miradi mikubwa unaofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli akidai kuwa inapelekea serikali kukopa fedha nyingi kutoka kwa wadau wa maendeleo na hivyo deni la taifa kuzidi kukua hali inayoweza kusababisha taifa kutokopesheka.

Nape ameyasema hayo jana bungeni katika kikao cha pili cha mkutano wa 9 wa bunge la 11 unaoendelea mjini Dodoma wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/2019.

Nape amesema kuwa hadi sasa kiwango cha serikali kukopa kimefikia asilimia 32 huku deni la taifa likiwa ni dola bilioni 26 na kusema kuwa miradi mikubwa inayotekelezwa huenda ikapelekea serikali kukopa dola 21 bilioni na hivyo kufanya deni la taifa kuwa dola 47 bilioni wakati ukomo wa kukopa ni dola bilioni 45.

Miongoni mwa miradi ambayo Nape ameikosoa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR), mradi wa kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) pamoja na mradi wa kufua umeme wa Stieglers Gorge katika maporomoko ya Mto Rufiji mkoani Pwani.

Nape ameeleza kuwa endapo serikali itaendelea kukopa ili kufadhili miradi hiyo, italazimika kutumia fedha kutoka sekta nyingine kulipia madeni hayo, jambo ambalo litakuwa likiumiza sekta hizo.

Aidha, mbunge huyo alisema, kutokana na miradi inayotekelezwa sasa na serikali ya awamu ya tano kuwa ya muda mrefu, serikali italazimika kuanza kulipa madeni iliyokopa kutekeleza miradi hiyo kabla ya miradi yenyewe kuanza kuwanufaisha wananchi, jambo ambalo litaifanya serikali kuchukua fedha kidogo ambazo zinatokana na kodi za wananchi kulipa madeni.

Katika hatua nyingine, Nape ameishauri serikali kuachana na utaratibu wa kutaka kufanya kila kitu yenyewe, badala yake itengeneze mazingira mazuri kwa ajili ya sekta binafsi kukua, ili kuepusha serikali kutumia fedha zote inazokusanya katika miradi ya ujenzi wa miundombinu, kuzalisha umeme, shughuli ambazo zingeweza kufanywa na sekta binafsi.
SOURCE: Mpekuzi

No comments