Header Ads

Mwanza Wazindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa......Waapa Kuipiku Dar es Salaam


Mkoa wa Mwanza umezindua mwongozo wa uwekezaji ukiweka mikakati ya kuupiku Dar es Salaam katika uchangiaji wa pato la Taifa.

Mwongozo huo umeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ESRF), kwa ufadhili wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema jana Jumatatu Novemba 27,2017 kuwa fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo, uvuvi, madini, viwanda na biashara ndizo zitatumika kuipiku Dar es Salaam.

“Tumejipanga kuongeza mchango wa Mkoa wa Mwanza katika pato la Taifa kutoka Sh7.4 trilioni za sasa hadi zaidi ya Sh10 trilioni kwa mwaka ifikapo 2025 kulingana na dira ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo muda huo,” amesema Mongella.

Mtaalamu kutoka ESRF, Dk Bohela Lunogelo amesema pato la mwananchi wa Mkoa wa Mwanza ni zaidi ya Sh2 milioni kwa mwaka.

Mongella amesema mkoa utaunda timu maalumu ya wataalam kutoka mamlaka, taasisi na idara za Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali na leseni ili kuwapunguzia wawekezaji urasimu wa kimfumo, hasa vibali na leseni za kuanzisha biashara.

“Hatulengi kuvunja kanuni na utaratibu; lakini hatuna budi kuchukua uamuzi pale urasimu wa kimfumo unapokuwa kikwazo kufikia malengo yetu ya maendeleo,” amesema Mongella.
By, MPEKUZI

No comments