Header Ads

Rais Magufuli asaini nyaraka za wafungwa walioachiwa huru

Rais John Magufuli ametia saini nyaraka za msamaha alioutoa kwa wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na wawili Nguza Viking (Babu Seya) na Johnson Nguza (Papii Kocha) waliohukumiwa kifungo cha maisha jela.Rais Magufuli ametia saini nyaraka hizo leo Jumapili Desemba 10,2017 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.Msamaha huo aliutoa jana Jumamosi Desemba 9,2017 katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara).Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri ya kurekebisha tabia za wafungwa.Taarifa ya Ikulu imesema Rais Magufuli amesisitiza kuwa pamoja na kutolewa msamaha huo, vyombo vya dola viendelee kusimamia sheria.

Amelitaka Jeshi la Magereza kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha mali, yakiwemo mazao ya kilimo na kufanya kazi za ujenzi.“Nimeona nitumie kifungu hiki cha Katiba -Ibara ya 45 (1) ambacho nilipewa na Watanzania, ingawa kilikuwa hakijawahi kutumika, unajua mtu ambaye alihukumiwa kunyongwa halafu baadaye anaachiwa, ni kitu kinashangaza kwa sababu hakijawahi kutokea, lakini nimeona nifanye hivyo kwa ajili ya Watanzania,” amesema.Rais Magufuli amesema, “Muendelee kusimamia wajibu wenu na kusimamia sheria, mtu anayehukumiwa kufungwa afungwe kweli, na nilishatoa wito kwa magereza, pasiwepo wafungwa wa kukaa tu na kupumzika, wafanye kazi, kufungwa si kustarehe.”Akizungumzia hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza Dk Juma Malewa amemshukuru Rais kwa kutoa msamaha huo wa kihistoria.Amesema wafungwa na maofisa Magereza wameipongeza hatua hiyo ambayo itasaidia kuwatia moyo wafungwa wanaorekebishwa tabia katika magereza nchini.Kamishna Jenerali Malewa amesema wafungwa waliopatiwa msamaha wa kuachiwa huru, waliruhusiwa kutoka magerezani tangu jana.Amesema maofisa Magereza wamewaasa kwenda kuonyesha mfano bora kwenye jamii watakakokwenda kuishi.Wakati huohuo, Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza agizo lake la kutengeneza viatu kwa ajili ya askari badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.Jeshi la Magereza linazalisha jozi 150 za viatu kwa siku katika kiwanda cha Karanga kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.Kwa kushirikiana na mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF, jeshi hilo limeanza kuboresha kiwanda hicho ili kufikia uzalishaji wa jozi 450 kwa siku.

Mwananchi:

No comments