Header Ads

AKAMATWA AKISAFIRISHA DOLA ZA MAREKANI 123, 000 BILA UTARATIBU

Jeshi la Polisi nchini limemnasa mfanyabiashara wa vipuri vya magari akiwa na Dola za Marekani 123,000 (Sh. milioni 274.4) kabla hajaingia kwenye ndege aliyokuwa anasafiri nayo kwenda Dubai.Kamanda wa Viwanja vya Ndege, Matanga Mbushi, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa 9:30 alasiri kwenye eneo la kuondokea 'Terminal II' la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.Akieleza zaidi kuhusu tukio hilo, Mbushi alisema polisi kwa kushirikiana na maofisa wa usalama na Mamlaka ya Mapato (TRA) walimkamata abiria huyo, aitwaye Boniface Mbilinyi (32) mwenye hati ya kusafiria AB 757247.
Alisema kuwa mfanyabiashara huyo ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea jijini alikuwa anasafiri kwa ndege ya Shirika la Emirates kuelekea Dubai kwa shughuli za kibiashara.
Kamanda Mbushi alibainisha kuwa mfanyabiashara huyo ni muuzaji wa vipuri vya magari, hivyo alikuwa anakwenda Dubai kununua vifaa hivyo.Alisema kiasi hicho cha fedha kimehifadhiwa kwenye akaunti ya Dola ya FIU yenye namba 20110028135, huju uchunguzi ukiendelea zaidi.

No comments