Header Ads

JESHI LA POLISI LINAWASHIKILIA POLISI SITA KUHUSIANA NA KIFO CHA MWANACHUO WA CHUO CHA NIT

Jeshi la polisi linawashikilia askari wake sita na silaha zao kwa ajili ya uchunguzi kuhusu tukio la kuuawa kwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akweline.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hayo leo Februari 18,2018 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ulinzi wakati wa kampeni, upigaji kura, na utangazaji matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni uliofanyika jana Februari 17,2018.
Kamanda Mambosasa amesema polisi iliunda timu ya upelelezi kuchunguza chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo kilichotokea Februari 16,2018 wakati polisi wakiwatawanya wanachama wa Chadema waliokuwa wanaandamana kwenda ofisi za mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kushinikiza mawakala wao kupatiwa barua za viapo vya kusimamia uchaguzi.
Kamanda Mambosasa amesema polisi pia inawachunguza watuhumiwa 40 ili kubaini iwapo miongoni mwao walikuwepo waliokuwa na silaha za moto.
Pia  amesema wanaendelea kuwatafuta wafuasi na viongozi wa Chadema walioshiriki kushawishi wafuasi wao kushiriki kwenye maandamano.  
Wakati huohuo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika taarifa aliyoitoa jana Februari 17,2018 alisema chama hicho kinalitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu aliyehusika na tukio la kuuawa kwa mwanafunzi huyo.
Polepole alisema polisi imhoji Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake walioshiriki maandamano aliyosema hayakuwa halali yaliyosababisha uhai wa Mtanzania kupotea.

No comments