Header Ads

MKUU WA MKOA WA ARUSHA KUTUMA TIMU KWA WAMILIKI WA MAKAMPUNI, MASHIRIKA NA TAASISI BINAFSI MKOANI ARUSHA.

   Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw.Mrisho Mashaka Gambo amewataka wamiliki wote wa makampuni, Mashirika na taasisi za sekta binafsi mkoani Arusha kuwa Februari 15, 2018 atatuma timu maalumu kwenye ofisi hizo kwa lengo la kuangalia, kuhakikisha na kutathmini jinsi sheria za kazi zinavyotekelezwa.
   Katika barua yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa Februari 12, 2018 Bw.Mrisho Gambo ameandika kuwa lengo la kuundwa kwa timu hiyo ni kutoa elimu na kuangalia usalama mahala pa kazi  ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora, wezeshi na endelevu kwenye sekta binafsi katika utekelezaji wa majukumu ya kazi kati ya waajiri na waajiriwa  mkoani Arusha zinalindwa na kuzingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha taasisi husika zinazingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi yetu.
   Ameongeza kuwa kupitia utaratibu alioanzishwa  wa kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa mkoa wa Arusha wa kila Jumanne na Alhamis kupitia dawati la mkoa na Mkuu wa mkoa mwenyewe pamoja na changamoto zingine ikiwemo migogoro kazini imekuwa ikitajwa na wananchi wengi kama changamoto kubwa.
   Bw.Mrisho Gambo ameongeza kuwa wameona ni busara kwenda kwenye maeneo husika ya kazi na kurekebisha changamoto hizo.
   Hata hivyo sekta binafsi wametaja  baadhi ya changamoto ambazo ni kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku mahala pa kazi ikiwemo kukosa mikataba ya ajira, mikataba isiyo na maslahi kwa wafanya kazi, wafanyakazi kuachishwa kazi kinyume cha utaratibu.
   Hivyo kutokana na uzoefu walioupata na kusikiliza mashauri mbalimbali ya migogoro kazini, wameona  ni busara kuunda timu hiyo itakayopitia taasisi zote binafsi ili kufuatilia masuala yote yanayohusu changamoto za wafanyakazi wa sekta binafsi mkoani Arusha na kuahidi kuwa watafanya usuluhishaji kwa njia za utawala na yakishindikana watayaacha yaendelee kwa mtiririko wa kimahakama lakini kwa kufuata na kuheshimu utawala wa sheria.

No comments