Header Ads

Trafiki arekodiwa akipewa rushwa 5,000/-, atimuliwa



Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Muliro J. Muliro amefunguka na kusema kuwa wamemchukulia hatua za kinidhamu askari polisi wake mmoja ambaye jina lake halijawekwa wazi kufuatia kuonekana akichukua rushwa kwenye video za mitandaoni.

Hatua hiyo ya jeshi la polisi imekuja masaa kadhaa baada ya Mwanaharakati wa mambo ya siasa mtandaoni, mrembo Mange Kimambi kuposti video ya askari polisi akichukua rushwa ya pesa kutoka kwa raia ambaye alitenda kosa la barabarani.

Katika tukio hilo, dereva mmoja aliyeombwa rushwa alimrekodi askari huyo kupitia simu yake ya mkononi wakati akimpatia rushwa hiyo iliyowekwa chini ya leseni.

Dereva huyo akiwa ametegesha kamera yake kwenye gari, askari huyo alifika kwenye kioo cha mlango wa dereva na kumrudishia leseni yake ambayo alikuwa nayo tayari, kisha askari huyo kumwomba ampatie leseni hiyo kwa mara nyingine ikiwa na rushwa.

Baada ya dereva kurudishiwa leseni, aliiunganisha na Sh. 5,000 aliyoiweka kwa chini na kumrudishia askari ambaye naye alikuwa akijifanya kama anatoa risiti kwenye mashine yake kielektroniki aliyokuwa ameishika mkononi.

Baada ya kupokea leseni iliyokuwa ikiwa imeambatanishwa na fedha hizo, trafiki huyo alichukua fedha na kumrudishia leseni dereva huyo kisha kuondoka.
 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi Jumanne Murilo,  amesema  tayari askari huyo ameshachukuliwa hatua kwa kufukuzwa kazi tangu Jumanne.

Kamanda Murilo alisema askari huyo hadi anafukuzwa kazi ndani ya Jeshi la Polisi alikuwa amefanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

"Tukio hili lilifanyika eneo la Mwenge na baada ya kulibaini tulianza uchunguzi wetu ambao juzi (Jumanne) ulikamilika na kubaini tukio hilo lilikuwa la kweli (kwamba) amepokea rushwa. Hivyo tumemuondoa kazini," alisema.

Kamanda Murilo ambaye hakumtaja jina askari huyo aliwakumbusha trafiki kuzingatia maadili ya kazi na taratibu za kijeshi zilizowekwa.

No comments