BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI KUTUMIA UKUMBI WA BUNGE DODOMA
Bunge la Afrika Mashariki (Eala) linakusudia kutumia majengo ya Bunge mjini Dodoma kufanya mkutano wake Aprili mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza tangu lianze majukumu yake mwaka 2001.
Spika wa Bunge la Eala,Martin Ngoga amelitangazia Bunge kuwa ameshawasiliana na Spika wa Bunge la Tanzania,Job Ndugai na ametoa kibali kwa ajili ya tukio la kihistoria ikizingatiwa katika kipindi hicho bunge la muungano litakuwa likiendelea na vikao vyake.
"Napenda kuwafahamisha kikao kijacho cha Bunge kitafanyika mjini Dodoma, itakuwa fursa ya kihistoria kwa sababu na wenzetu watakuwa kwenye vikao vya Bunge itatupa nafasi ya kujenga uhusiano wa kiutendaji na kuimarisha jumuiya yetu," amesema Ngoga.
Kwa mujibu wa taratibu za Bunge la Eala hufanya vikao vyake kwa mzunguko kwenye miji mikuu ya nchi wanachama na hapa nchi vikao vimekuwa vikifanyika jijini Dar es Salaam na Zanzibar kama sehemu ya muungano wakati Arusha hutambulika ni makao makuu ya EAC.
Bunge la Afrika Mashariki linaundwa na wabunge 54 kutoka nchi sita wanachama ambao ni Tanzania,Kenya,Uganda,Rwanda,Burundi na Sudani Kusini pia wajumbe wanane ambao ni mawaziri wanaohusika na EAC, Katibu Mkuu wa EAC na Mwanasheria wa EAC.
Mbunge wa Bunge hilo kutoka Tanzania, Happiness Lugiko alipongeza uamuzi wa Spika kufanya vikao vyake mjini Dodoma."Jumuiya ya Afrika Mashariki imeanzishwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wetu vyema, kufanya vikao vyetu huko ni jambo zuri na tunaliunga mkono pamoja na sababu nyingine pia linalenga kuwafanya wananchi wa Dodoma wazifahamu kazi zetu," amesema Lugiko.
Afisa Habari Mwandamizi wa Eala,Bobi Odiko amesema mipango ya kufanya vikao vyao mjini Dodoma imeshakamilika licha ya Bunge la Muungano kuwa na vikao vyao katika kipindi hicho watatumia ukumbi mwingine kw aajili ya kutimiza majukumu yao kuanzia Aprili 3 hadi 22 mwaka huu.
Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Eala ni Adam Kimbisa, Josephine Lemoyan, Happiness Lugiko, Pamela Maassay, Dk Ngwaru Maghembe, Dk Abdullah Makame, Habib Mnyaa, Fancy Nkuhi na Maryam Ussi Yahya.
No comments