Header Ads

HUKUMU YA BABU SEYA NA PAPII KOCHA KUSOMWA LEO

Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) leo Ijumaa Machi 23, 2018 itasoma hukumu ya kesi ya wanamuziki wa dansi, Nguza Viking maarufu Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.

Wanamuziki hao walikata rufaa iliyosajiliwa na kupewa namba 006/2015 katika mahakama hiyo kupinga kifungo cha maisha.

Wakati hukumu hiyo ikitarajiwa kusomwa leo, Babu Seya ambaye ni mtunzi wa kibao maarufu cha “Seya” na Papii Kocha ambaye wameshirikiana katika wimbo huo ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika, Desemba 9, 2017.

Walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa na adhabu za vifungo vya maisha na kunyongwa ambazo si rahisi kupata msahama wa kawaida wa mkuu wa nchi unaotolewa siku ya sherehe hizo.

Rais wa mahakama hiyo, Jaji Sylvian Ore alisema mahakama itasoma hukumu hiyo baada ya kukamilisha mahitaji yote na kupata taarifa za wakata rufaa.

Hata hivyo, wakati Jaji Ore akiahirisha kusoma hukumu hiyo, wanamuziki hao hawakuwepo mahakamani.

Baadhi ya mawakili waliokuwepo mahakamani hapo wamesema licha ya kuwa wanamuziki hao wamepata msamaha wa rais, hukumu yao itasomwa.

"Mahakama hapa itatoa hukumu ili kuweka rekodi za kimahakama katika kesi za aina hii na hata kama ikieleza walikuwa na hatia haina athari kwao,” amesema wakili Daniel Kalasha.

Katika kesi hiyo, Jamhuri inawakilishwa na mawakili Sara Mwaipopo na Nkasori Sarakikya.

No comments