Header Ads

JAMII YATAKIWA KUTUMIA ARDHI KWA TIJA NA KWA UBORA.

Na Paschal D.Lucas
paschald.lucas@gmail.com
Arusha

Hayo yamesemwa na Bi.Albina Bura Mkurugenzi msaidizi tume ya Taifa ya kupanga matumizi bora ya ardhi kutoka  Dar Es Salaam na mratibishi wa mafunzo ya matumizi bora ya ardhi alipokuwa akiongea wakati wa semina ya mafunzo ya matumizi bora ya ardhi kwa maafisa kilimo, ardhi, mifugo, mipango na wadau mbalimbali wa Ardhi wa Halmashauri za wilaya ya Arusha Dc na Meru katika ukumbi wa Gymcana Arusha.

Bi.Albina Bura amesema kuwa mafunzo hayo ya siku tano yana lengo la kusaidia kujenga uwezo wa wataalamu wa wilaya ya Arusha ili waweze kuandaa mipango bora ya matumizi ya ardhi kwa vijiji ambavyo viko kwenye Wilaya hiyo.

Ameongeza kuwa suala la kupanga matumizi bora ya ardhi limepewa nguvu kisheria  kwa sheria namba 6 ya mwaka 2007  ya matumizi bora ya ardhi ya taifa.
Aidha amesema kuwa lengo la tume hiyo nikuhakikisha kwamba inatoa elimu kwa wataalamu wa wilaya wajue hatua ambazo zinatakiwa kupitia ngazi ya wilaya  na kuhakikisha kwamba baadae waende kupanga mipango kwenye vijiji.

Hivyo amesema kuwa baada ya mafunzo hayo wamepanga kufanya mafunzo kwa vitendo na kwa uhalisia kwa kijiji kimoja kama mfano ili kujikamilisha kabisa kwa elimu hiyo na baadae waendelee kwa vijiji vingine vilivyomo kwenye wilaya yao.

Akitoa wito kwa washiriki na jamii kwa ujumla juu ya mafunzo hayo  kwa niaba ya mkurugenzi wa tume hiyo  kuwa  mpango huu wa matumizi ya ardhi unaanzia ngazi ya taifa mpaka mtu binafsi hivyo mpango uko tayari na umeshaandaliwa tangu mwaka 2013 na utatumika mpaka mwaka 2033  hivyo jamii ielewe kutumia kwa usahihi na kwa ubora ardhi na rasilimali zilizoko kwenye ardhi kwa kuvitunza kwa matumizi  vizazi vilivyopo na vijavyo.

Naye Elisha Sanaa ambaye ni Afisa kilimo wa wilaya ya Arusha Dc ameshukuru kwa mafunzo hayo na kusema kuwa mafunzo hayo ni ya msingi sana kwa wataalamu wa kilimo na wananchi kwa ujumla hususani wakulima na wafugaji hivyo yatasaidia kujitambua kwa kupangilia sehemu za kulima na kufungia mifugo na kwa kuyatunza mazingira kwa tija na si vinginevyo.

Bw.Elisha Sanaa ameongeza kuwa mpango huu wa matumizi bora ya ardhi unaainisha bayana maeneo kwa kutambua baina ya mipaka kati ya kijiji na kijiji, makazi na miundombinu na hivyo ardhi inatakiwa kutunzwa kwani kupitia mafunzo hayo yatamsaidia kuelimisha wananchi hasa wa wilaya ya Arusha Dc kwa kuwahimiza na kusisitiza matumizi mazuri na bora ya ardhi kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia mafunzo hayo Afisa mifugo wa wilaya ya Arusha Dc Bi.Epifania Dornald Swai amesema kuwa kupitia mafunzo hayo ya matumizi sahihi na bora ya ardhi yatamsaidia katika kuelimisha jamii hususani wafugaji kwa kuwapa mbinu ya ufugaji bora kulingana na ukubwa wa eneo na idadi ya mifugo kwa kuwashauri wafugaji wafuge kisasa ufugaji wenye tija na faida  kwa kuwa na idadi ndogo ya mifugo ili kupunguza uharibifu wa mazingira na rasilimali zilizoko kwenye ardhi na kusababisha mmomonyoko wa udongo hivyo kusababisha upotevu wa rutuba kwa ardhi.

Mafunzo hayo ya matumizi bora ya ardhi yatafanyika kwa siku tano ambapo siku ya ijumaa ya tarehe 16, Machi itakuwa siku ya kilele cha mafunzo hayo.

No comments