MWANZA, KAMANDA WA POLISI AWASISITIZA ASKARI KUEPUKA UBAMBIKAJI KESI.
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi amewasisitiza askari
kuepuka ubambikaji kesi kwa wananchi, rushwa na ubabaishaji pia akiwataka
askari kufanya kazi kwa utii, nidhamu na maadili kama ambavyo Jeshi la Polisi
Tanzania linavyoelekeza. Hayo yamejiri tarehe 28/02/2018 wakati Kamanda Msangi
alipokutana na askari wa Wilaya ya Sengerema katika ukaguzi anaoendelea
kuufanya katika Wilaya na Vikosi vyote hapa Mkoani Mwanza.
Amewataka askari
kukomesha vitendo vya ubabaishaji kwa wananchi na ubambikaji kesi kama vipo,
mfano kesi ya madai inabadilishwa kuwa kesi ya jinai jambo ambalo linanyima
haki wananchi na kuchafua sifa nzuri ya Jeshi la Polisi. Hivyo ubabaishaji wa
aina hiyo uepukwe na yeyote atakaye bainika anafanya hivyo hatua za kinidhamu
zitachukuliwa dhidi yake.
Sambamba na hilo
Kamanda Msangi amewataka askari wa kila kitengo kusimama vyema katika nafasi
zao, ambapo alisema kila askari akiwa vizuri katika utendaji kazi hakutakuwa na
malalamiko yeyote toka kwa wananchi hivyo ni jukumu la kila askari kuhakikisha
dhamana aliyopewa na serikali ya kulinda wananchi pamoja na mali zao anaisimamia vizuri bila ubabaishaji wa aina
yeyote ile.
Pia aliwataka askari
wawe na utaratibu mzuri wa upokeaji, utunzaji na uondoshaji wa vielelezo katika
vituo vya Polisi, kwani katika baadhi ya vituo vya Polisi lipo tatizo la
utunzaji wa vielelezo hivyo hataki kuona tatizo hilo linaendelea kuwepo.
Vilelele aliwataka Maofisa wa Polisi wa Wilayani hapo kuzingatia taratibu
zilizowekwa kisheria za uondoshaji wa vielelezo katika vituo vya Polisi.
Hata hivyo alisema
hategemei kuona mlundikano wa vielelezo katika vituo vya Polisi ambavyo vimekaa
vituoni mwaka mmoja au zaidi. Kwani madhara yake vinaweza kuharibika, kupoteza
ubora au kupotea alafu baadae liwe deni kwa Jeshi. Hivyo aliwataka askari
kutekeleza maamuzi ya mahakama haraka juu ya uondoshaji wa kielelezo/vielelezo
baada ya kesi kumalizika mahakamani.
Kwa upande wa
upelelezi alisema kumekuwa na tatizo la kuchelewesha upelelezi wa kesi nyingi.
Jambo ambalo linawanyima wananchi haki. Hivyo alimtaka Mkuu wa Upelelezi Wilayani
hapo kushughulikia suala hilo mapema lisiwepo katika himaya yake ili haki
ipatikane haraka bila uonevu wa aina yeyote.
Pia aliwapongeza
askari wa Wilaya hiyo kwa utendaji mzuri wa kudhibiti uhalifu, aliwataka
waongeze juhudi kwa yale maeneo yenye vibaka na uhalifu mwingine mdogomdogo
kwani anaamini wanaweza. Ushirikiano ulipo na Viongozi wa ulinzi na usalama
Wilaya, Wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama udumishwe ili
Sengerema iwe salama zaidi kwani amani ikiwepo maendeleo yatapatikana zaidi.
No comments