Header Ads

WAZIRI MWIGULU NCHEMBA APONGEZA JUHUDI ZA BODABODA ARUSHA NA KUWAUNGA MKONO KWA MILIONI 10

Na Paschal D.Lucas
Waziri wa mambo ya ndani Mh.Mwigulu Nchemba amepongeza juhudi na hatua ya umoja wa bodaboda jiji la Arusha(UBOJA) kwa kushirikiana na mkuu wa Mkoa huo Mrisho Gambo kwa hatua kubwa ya kuimarisha umoja wa waendesha bodaboda mkoani humo.
Akitoa pongezi hizo mbele ya mkuu wa mkoa, viongozi wandamizi wa mkoa na umoja wa waendesha bodaboda wa Arusha kwenye kikao cha kuwakabidhi vijana bodaboda kilichofanyika leo Machi 3,2018 katika ukumbi wa Mount Meru Hotel jijini Arusha.

Naye Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani wa mkoa (RTO) aliyefahamika kwa jina moja la Bw.Bukombe amesema kuwa waliohitimu mafunzo hayo ni jumla ya vijana 250 kwa wiki iliyopita na wengine zaidi ya mia moja(100) wanatarajia kumalizia mafunzo yao siku ya jumatatu.
Bw.Bukombe ameunga mkono wazo la Mkurugenzi wa mamlaka ya mapato( TRA) mkoa kwa kuwataka kuingia darasani wapate mafunzo ili waweze kupata vyeti na leseni kwa njia sahihi.
Ameongeza kuwa bodaboda wanatakiwa kuvaa kofia ngumu na kuwa wasafi kwa abiria wao na waachane na suala la ubebaji wa mishikaki na kuheshimu alama za barabarani ikiwemo sehemu za wavuka miguu.

 Mwenyekiti wa umoja wa bodaboda jiji la Arusha(UBOJA) Bw.Maulid Makongolo mezitaja changamoto wanazozipata wakati wa uendeshaji wa bodaboda jijini humo wakati akisoma risala mbele ya Waziri Lazeck Nchemba kuwa ni pamoja na ulemavu na vifo kwa sababu ya ajali, kutekwa na kunyang’anywa pikipiki na kupigwa,upinzani wa kisiasa, baadhi ya viongozi kutotambua wanapohitaji msaada, na baadhi yao kutokuwa waaminifu katika marejesho.
Alitaja pia malengo yao ni pamoja na kujua idadi halisi ya waendesha pikipiki,kufungua miradi ya umoja,mfuko wa kusaidiana na kushiriki shughuli za kijamii.
Baada ya mwenyekiti wa Umoja wa bodaboda jiji la Arusha kusoma risala mbele ya waziri wa mambo ya ndani Mh.Mwigulu Nchemba Mkuu wa wilaya ya Arusha Bw.Gabriel Ndakaro  alisema pikipiki zilizotolewa kwa waendeshaji hazikuwa na riba  wala dhamana na sababu ya kutoa pikipiki hizo ni kwa sababu ya wazi kabisa kuwa waendesha bodaboda ni watu wanyonge hivyo wasingeweza kupata mkopo benki na baadhi ya wanasiasa kuwataka wasipaki na waondoke maeneo ya benki na wasiingie mjini kabisa.
Lakini kupitia juhudi za viongozi walipambana na suala hilo na halikuweza kutokea.Amewataka waweke utaratibu wa kuhakikisha bodaboda wote waliosajiliwa kwenye umoja huo kutii na kufuata taratibu zote za sheria ili kuimarisha umoja wao na kuleta ushikamano baina ya serikali na waendesha bodaboda.
Akimkaribisha Mh.Mwigulu Nchemba Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw.Mrisho Gambo amemshukuru Mh.Waziri Mwigulu Nchemba kwa kukubali kushiriki zoezi hilo na kuwashukuru watendaji wa ngazi zote kuanzia mkuu wa wilaya, watendaji na maafisa tarafa kwa kusimamimia zoezi la ukusanyaji wa pesa kufanikisha zoezi hilo na kuwataka watendaji kwenda kushiriki kutatua kero za wananchi kama walivyoagizwa na serikali ya awamu ya tano.
Bw.Mrisho Gambo amewataka wananchi wa Arusha kuwa hakuna suala la maandamano tena mkoani humo kwa sasa kama ilivyokuwa imezoeleka zamani kwa viongozi wa vyama pinzani kuwatumia bodaboda kuanzisha maandamano hayo.
Ameongezea kuwa si kwa sasa kwani sasa hivi ni muda wa kazi kutatua changamoto na kero  za wananchi nakuleta maendeleo na itabaki kuwa ni historian a kuwahakikishia kuwa wamejipanga vizuri.

“Nataka niwahakikishie kwamba sisi  tumejipanga vizuri, mtu yeyote kwa sababu yeyote ambaye atatumwa kuja kupima kina cha maji tutamsaidia kuzama” Alisema

Alisisitiza suala la siasa kuwa tunataka siasa yenye kuleta maendeleo na sio kubomoa kama ilivyokuwa imepangwa kwa bodaboda kutoingia mjini bali waishie nje ya mji.
Bw.Mrisho Gambo alielezea pia suala la maendeleo ya mkoa kuwa mpaka sasa wameanzisha ujenzi wa vituo vya afya katika kata mbalimbali na Mh Rais Magufuli ametoa zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wab Arusha.

Akijibu risala Mh.Lameck Nchemba amewataka vijana kujiepusha na makundi mabaya yanayoleta uvunjifu wa amani nchini huku akiwataka waepukane na ajali kwa kuzingatia taratibu za uendeshaji wa bodaboda kwa kufuata alama zilizoko barabarani na kuhakikisha kuwa kila mwendesha bodaboda awe na kofia ngumu mbili za kuendeshea pikipipiki kwa maana ya dereva na abiria.

Mh. Mwigulu Nchemba amewashukuru watendaji na viongozi wa ngazi zote za kijiji,kata, wilaya mpaka mkoa kwa juhudi zao za kuleta maendeleo hususani kwa suala la ajira kwa vijana kwa kuwaunganisha na kuwasaidia vijana kujiajiri kupitia kazi ya uendeshaji wa pikipiki(Bodaboda) kwa kushirikiana na mkuu wa mkoa ambaye ni alama ya uaminifu na utendaji kazi kwa ngazi ya mkoa.

“Serikali ya awamu ya tano chini ya Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli imetuamini vijana kwa sababu ya utendaji na uwajibikaji wetu kwa taifa, hivyo kupitia muunganiko huu na ushirikiano huu wa viongozi wa ngazi zote na mkuu wa mkoa unatufanya tuzidi kuonekana na kuaminika kwa taifa kuwa vijana tunaweza kiuntendaji” Alisema

Mh.Mwigulu Nchemba amewataka wamiliki na waendeshaji wa bodaboda kufuata taratitu zote za umiliki wa pikipiki kwa kuhakikisha kuwa pikipiki inakuwa na kofia mbili kwa dereva na abiria,leseni na kadi ya pikipiki ndipo ihesabike kuwa imekamilika na  kuondokana na ukamataji usio na heshima na kuleta umoja ulio imara.
Mh.Mwigulu Nchemba amelitaka na kulikumbusha Jeshi la Polisi nchini kuwa pikipiki ambazo zina makosa madogomadogo zilizoko vituoni zirudishwa kwa wenye nazo  wakazirekebishe kuepukana kuwa chuma chakavu, lakini kwa pikipiki zenye makosa yanayohitaji upelelezi na ushahidi ziendelee kubaki kwenye vituo vya Polisi.
Ameongezea pia kuwa kila dereva boda boda ahakikishe anavaa kofia na abiria wake.

“Kila pikipiki iwe na kofia mbili moja ya dereva na nyingine ya abiria,kama abiria hatavaa ni kosa la abiria na sio mwendeshaji, na kama pikipiki ina kofia moja tu ya dereva ni kosa la mwenye bodaboda hivyo faini italipwa na aliyetenda kosa hilo” Alisema

Mh.Mwigulu Nchemba ameridhia ombi la mkuu wa mkoa la kuwapa miezi mitatu waendesha bodaboda bila kukamata na kuongezea kuwa kuna utaratibu wanaratibu pawepo na usawa  baina ya faini ya pikipiki na gari zingine kama costa nasio uliopo sasa hivi.
Amemalizia kwa kupongeza mkuu wa mkoa kwa kufanya mpango mkakati  wa kuwafanikisha bodaboda kufikia hatua hiyo na kuwaunga kwa mchango wa shilingi milioni kumi (10,000,000) ili kuongeza jitihada za kuwapa vijana pikipiki zingine ili wajikwamue kimaisha.
Umoja wa bodaboda jiji la Arusha (UBOJA) ulianzishwa rasmi mwezi Disemba 2016 ukiwa na wanachama 200 mpaka sasa wako jumla ya wanachama 500.




No comments