Header Ads

Rais Trump amfuta kazi Rex Tillerson, amteua Mike Pompeo

Washington, Marekani.  Rais Donald Trump amefuta kazi Waziri wa wa Mambo ya Nje, Rex Tillerson na amemteua Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) Mike Pompeo.
"Mike Pompeo, ambaye ni mkurugenzi wa CIA, atakuwa waziri wetu wa mambo ya nje.
Atafanya kazi vizuri sana," amesema Trump kwa njia ya Twitter Jumanne.
"Nakushukuru sana Rex Tillerson kwa huduma uliyoitoa!" ameongeza rais.
Shirika la Habari la CNN limesema nafasi ya Pompeo inatarajiwa kuchukuliwa na Gina Haspel.Tillerson, Jumatatu alilazimika kukatisha ziara yake ya kwanza ndefu barani Afrika kwa kile kilichoelezwa kwamba kazi nyingi.“Kutokana na mahitaji katika ratiba ya waziri, anarudi Marekani mapema baada ya kukamilisha ziara ya kiserikali Chad na Nigeria,” amesema msaidizi wake Steve Goldstein.
Tillerson aliyeanza ziara ya Afrika Jumatano alirudi Marekani baada ya kutembelea Ethiopia, Djibouti na Kenya ambako ilielezwa aliugua kwa muda.
Kwa mujibu wa CNN, Trump alimtaka Tillerson kujiuzulu nafasi hiyo tangu Ijumaa wakati akiwa katika ziara ya nchi kadhaa za Afrika.
Shirika hilo limemnukuu ofisa mmoja wa utawala akisema Trump alimtaka Tillerson ajiuzulu ili nafasi hiyo ichukuliwe na mtu mwingine. Ofisa huyo amesema rais anaona huu ni wakati mwafaka kufanya mabadiliko hasa kutokana na mazungumzo yanayokuja na Korea Kaskazini na majadiliano mbalimbali kuhusu biashara.
Muda mfupi baadaye Pompeo alitoa shukrani zake kwa Rais Trump. “Namshukuru sana Rais Trump kwa kuniruhusu kuhudumia kama Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la CIA na kwa kunipa fursa ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Uongozi wake umeifanya Marekani kuwa salama na natazamia kumwakilisha yeye na watu wa Marekani katika ulimwengu kwa ajili ya ustawi wa Marekani.”

No comments