Header Ads

China yatoa msaada 29.4bilioni



Serikali ya China imeipatia Tanzania msaada wa Shilingi 29.4bilioni kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu, utalii wa kijiolojia na kuukarabati Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango  Doto James, kwa niaba ya Serikali, na Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Gou Haodong.
Katibu huyo amesema 22.4bilioni  zitatumika kujenga Chuo cha Ufundi Stadi-VETA wilayani Ngara mkoani Kagera.
“Fedha hizo zitatumika kujenga vyumba 19 vya madarasa, ujenzi wa karakana 9 za kutolea mafunzo ya elektroniki, ufundi bomba, useremala, ufundi uashi na upakaji rangi” amesema   James

Ameeleza kwamba  kiasi hicho pia kitatumika kujenga majengo ya utawala, mabweni, nyumba za walimu na miundombinu mingine itakayosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye chuo hicho.
“Tunaamini kwamba msaada huo utakuwa sehemu ya kusaidia jitihada za Serikali za kujenga uwezo wa wataalamu wake watakaochangia kukuza sekta ya uzalishaji na hatimaye kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini” amesema  James
Katibu Mkuu huyo amesema China, itatoa 6.7bilioni kwa ajili ya kuukarabati Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

“Katika makubaliano yetu ya msaada wa kuendeleza Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000, China itatoa msaada wa kiufundi na vifaa vya kisasa vya michezo na utaalamu katika usimamizi na ukarabati wa uwanja” Amefafanua James

Amesema  kiasi kingine cha shilingi 300milioni zitatumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kuanzishwa kwa aina mpya ya utalii ujulikanao kama utalii wa kijiolojia “Geopark Project” katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, mkoani Arusha.
Alisema lengo la utafiti huo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na maajabu mbalimbali ya kitalii yaliyopo nchini ambayo hayajatumika kikamilifu kuvutia watalii watakaoongeza pato la Taifa
“Tanzania ina kila sababu ya kujifunza kutoka katika Hifadhi ya Kimataifa ya Jiolojia ya Jiaozuo ya Yuntaishan ya China, iliyoanzishwa mwaka 2000 ambayo inaongeza asilimia 37.2 ya watalii kila mwaka na huchangia asilimia 12 ya pato la Taifa la nchi hiyo” 
Tangu miaka ya 1960 mpaka sasa nchi hiyo imeendelea kuisaidia  Serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi, Ujenzi wa Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Gou Haodong, amesema ujenzi wa Chuo Cha Ufundi Veta huko Ngara mkoani Kagera utaanza haraka kama ilivyopangwa.
Kuhusu masuala  ya utalii wa kijiolojia katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, amesema Tanzania ina bahati ya kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini haijavutia idadi kubwa ya watalii kutoka China kuja kuvitembelea.
“Zaidi ya watalii milioni moja kutoka China wanatembelea nchi mbalimbali dunia lakini kati ya hao, Tanzania inapokea watalii 20,000 tu kila mwaka kutoka China, lakini kwa kuanzisha mradi huu, watalii wengi kutoka China watavutiwa kuja nchini kufurahia utalii wa miamba, mandhari nzuri, urithi wa dunia, na kutembelea hifadhi za Taifa” ameongeza Haodong
Akizungumzia masuala ya uchumi, Balozi huyo amesema  hivi sasa China imekuwa mwekezaji mkubwa zaidi nchini Tanzania kwa kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani 1.77bilioni  na kukuza ajira nchini.
Ameitaja baadhi ya miradi mikubwa iliyowekezwa kuwa ni pamoja na mradi wa miundombinu ya mtandao (Tanzania ICT broadband backbone), Bomba la gesi la kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi wa kuboresha miundombinu ya bandari ,barabara na madaraja.

No comments