Header Ads

Wadau wa habari nchini wainyooshea kidole Serikali



Wadau wa habari wamesema taasisi za kiraia, asasi na vyombo vya habari vinaogopa kutoa taarifa zinazoikosoa Serikali kwa kuhofia usalama na vitisho wanavyotoka kwenye mamlaka.
Mtafiti Mwandamizi wa Shirika la Twaweza, Annastazia Rugaba alizitaka taasisi na wadau wote wa utoaji taarifa kutoogopa vitisho, akitolea mfano wa vitisho walivyowahi kukutana navyo katika utoaji wa takwimu.
Kauli hiyo iliibuliwa jana kupitia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji Taarifa, yaliyokuwa yameandaliwa na Wadau wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni uamuzi wa Serikali kujiondoa katika Mpango wa Utendaji Kazi wa Serikali kwa Uwazi (OGP), kufungiwa kwa magazeti likiwamo la Mwanahalisi huku wakihoji maslahi ya viongozi katika utekelezaji wa taarifa na ucheleweshwaji kanuni za Sheria ya Kupata Taarifa.
Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Amiri Manento ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema haki ya kupata taarifa inatakiwa kulindwa kwa nguvu zote na kwamba, kuminywa kwake kuna athari katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, Absalom Kibanda alisema mazingira ya Serikali kunyima uhuru wa mtoa taarifa ni matokeo ya kuendelea kuongozwa na chama na viongozi waliopo katika mfumo unaohitaji kuzuia maovu yanayofanyika. Kibanda alisema Taifa lilitoka gizani, lakini sasa linapitia kipindi kingine kigumu.
Mwandishi nguli wa habari, Jenerali Ulimwengu alisema wanahabari wanaogopa kuuliza maswali wakiogopa kukamatwa na kupewa vitisho huku wanasiasa wa upinzani wakizuiwa kufanya mikutano ya hadhara kuwapatia taarifa wananchi kwa maagizo ya ‘amri kutoka juu’.
“Tumeingia kipindi cha ‘kujingishwa’, yaani tumeendelea kufanywa wajinga, suala la makinikia, Escrow vimeishia wapi, lakini kwa nini kuzuia mikutano ya kisiasa, hakuna sheria inayozuia wanasiasa wasifanye siasa ni kazi yao kutoa taarifa kwa njia hiyo, viongozi wanaogopa kuulizwa maswali na waandishi,” alisema Ulimwengu.
Awali, Mwenyekiti wa CoRI, Kajubi Mukajanga alisema kwa mara ya kwanza katika historia ya Taifai haijawahi kutokea uongozi uliowahi kukandamiza uhuru wa kupata habari kwa Watanzania.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye pia ni Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi hakuwa tayari kuzungumzia tuhuma hizo.

No comments