Header Ads

Madiwani wavutana Dodoma



Dodoma. Mvutano umeibuka katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma baada ya baadhi ya madiwani kubishana iwapo kikao ni cha dharura au maalumu.
Mabishano hayo yametokea baada ya sekretarieti kusoma ajenda mbili za kupokea taarifa ya ufungaji wa hesabu za mwaka na kupokewa mali za iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu ya Mji wa Dodoma (CDA).
Diwani wa Majengo (CCM), Mayaomayao Msinta amesema alipokea barua ya mwaliko kuwa ni kikao maalumu lakini walipofika wameambiwa ni cha dharura.
"Mtuambie ni kikao gani, maalumu au cha dharura? Barua inaeleza kikao maalumu lakini hapa tumesomewa ajenda mbili na kikao cha dharura kina kanuni, huwa na ajenda moja tu," amesema.
Diwani wa Nzuguni (CCM), Alloyce Luhega amesema makabrasha wamepewa leo Alhamisi asubuhi, hivyo itakuwa vigumu kujadili na kutoa mapendekezo kwa manufaa ya watu waliowachagua.
"Mimi nimepata taarifa leo asubuhi ni vigumu kujadili kwa sababu hatujasoma," amesema.
Akijibu hoja hizo, katibu wa baraza ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi amesema kikao hicho ni matokeo ya maazimio ya vikao vya mabaraza yaliyopita ambavyo viliamua kuwa baada yakupokewa mali za iliyokuwa CDA wapatiwe taarifa.
"Nawaomba tuendelee na kikao maana hata mkiuliza maswali hamtapata majibu maana sisi tumekabidhiwa. Isipokuwa tumepewa mapendekezo ya namna ya kutoa huduma kwa wananchi bila kukwama," amesema.
Amesema kuna watu walianza kulalamika kuwa manispaa imeanza kufanya kazi za iliyokuwa CDA kabla ya kukabidhi taarifa.
Amesema walilazimika kufanya baadhi ya kazi za iliyokuwa CDA ili kuondoa usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakihitaji huduma.
Meya wa Manispaa ya Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe amewasihi madiwani kuwa na busara katika kujadili jambo hilo.
Mvutano huo umemalizwa kwa kikao kuendelea baada ya madiwani kupiga kura. Madiwani 43 kati ya 46 wameridhia kikao kiendelee

No comments