Header Ads

Pingamizi la utetezi lazua mapya kesi ya mmiliki Lucky Vincent



Arusha. Kesi inayomkabili mmiliki wa Shule ya Lucky Vincent, Innocent Moshi na makamu mkuu wa shule hiyo, Longino Mkama imekwama kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru.
Hatua hiyo imetokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Desdery Kamugisha kuutaka upande wa Jamhuri kurekebisha hati ya mashtaka.
Awali, wakili wa utetezi, Method Kimomogoro aliweka pingamizi katika kosa la kwanza na la tatu yanayomkabili Moshi akidai hayana msingi wa kisheria.
Akisoma hati ya mashtaka mahakamani, Wakili wa Serikali, Alice Mtenga alitaja makosa manne yanayomkabili Moshi la kwanza likiwa ni kuruhusu gari aina ya Toyota Rossa kubeba wanafunzi bila ya kuwa na kibali. Kosa la pili ni kuruhusu gari kutembea barabarani bila kuwa na bima.

Mtenga alisoma kosa la tatu dhidi ya Moshi kuwa ni kushindwa kuwa na mkataba wa kazi akidaiwa Juni Mosi akiwa mmiliki wa gari hilo, alishindwa kumpatia mkataba wa kazi dereva Dismas Gasper na kosa la nne ni kuzidisha abiria 13 kwenye gari lililowabeba wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent.
Upande wa mashtaka ulimsomea Mkama shtaka la kuruhusu gari kubeba abiria kinyume cha sheriaakiwa msimamizi  wa shule hiyo.
Wakili Kimomogoro amesema kosa la kwanza dhidi ya Moshi halina msingi wa kisheria kwa kuwa hati ya mashtaka haijafafanua kwa kina endapo biashara hiyo ilikuwa ni ya kukodi au ujira. Kwa kosa la tatu amedai hati ya mashtaka haikutaja kifungu cha kanuni ya adhabu ambacho kimekiukwa.
Baada ya pingamizi, hakimu Kamugisha alitoa nafasi kwa upande wa Jamhuri kuzungumzia pingamizi hilo, ndipo Wakili wa Serikali Khalili Nuda aliposimama na kukiri katika kosa la kwanza hawakuainisha maneno kukodi au ujira lakini hilo halizuii hati ya mashtaka kutopokewa
Nuda amedai katika kosa la tatu kuwa, kesi ndiyo inaanza kusikilizwa mahakamani, hivyo upande wa Jamhuri bado unaweza kupewa muda wa kurekebisha hati ya mashtaka. Ameiomba Mahakama iwapatie muda kwa kuwa walikosea.
Hakimu Kamugisha ametoa uamuzi akikubaliana na hoja za pingamizi zilizotolewa na upande wa utetezi.
Ametoa amri kwa Jamhuri kwenda kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka. Ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 6

No comments