Header Ads

Maisha Ya Chuo

Untold story.Na Paschal D.Lucas













Ilikuwa mwaka 2014 pale nilipojiunga na chuo mwaka wa kwanza, tukiwa darasani tukisubiri mwalimu. Pembeni yangu alikaa msichana mmoja mzuri sana, alikuwa amevaa gauni lake fupi lililomkaa vema, kichwani alikuwa amesuka rasta zilizomfanya avutie sana. Sio siri alikuwa ni mrembo haswa!
Niliona si vibaya nikianza kumsemesha, nilimsalimia bila ajizi nae aliitikia, nikajitambulisha jina langu  kuwa Mimi ni Paschal D. Lucas na vinginevyo bila shida yoyote nae akaonesha ushirikiano mzuri, tuliongea muda mrefu sana kwani baadae kupitia kiongozi wa darasa tulipata taarifa kuwa mwalimu asingeweza kufika siku hyo. Kupitia maongezi hayo nilimjua kuwa alikuwa akiitwa Judith na alikuwa akiishi na wazazi wake huko Mwanza.
Basi mazoea yetu ndio yakawa yameanza rasmi, tulikuwa pamoja muda mwingi sana pale chuoni. Tulishirikiana kufanya assignements mbalimbali na kipindi karibia na mitihani tulisoma pamoja pia.
Binafsi nilikuwa nimepanga chumba maeneo ya Chemchemi hii ilitokana na baada ya kukosa pesa ya kulipia hostel chuoni, kwa upande wangu maisha hayakuwa mazuri hata kidogo, wazazi wangu huko mkoani hawakuwa na kipato kikubwa zaidi ya kujikimu na familia pamoja na mdogo wangu.
Hivyo nilivyokuja chuo nilijua ningepata hostel ili kupunguza gharama za accomodations ila bahati mbaya ndio hivyo nikakosa pesa ya kulipia. Ikanibidi nitafute chumba cha bei rahisi ndio nikapata huko Chemchemi maeneo ya uwanja wa Ali H.Mwinyi Tabora.
Ndani nilikuwa na godoro lilowekwa chini kwani Sikuwa na kitanda, pia kulikuwa na meza ya kusomea kiti, ndoo 2 za  maji na jiko la mchina na vyombo kadhaa.
Maisha ya chuo yaliendelea, semister zilikatika na mazoea na Judith yalizidi kiwango, hatukujua ni nini kilitokea kati yetu ila mwisho wa siku tukajikuta tukiwa wapenzi. Nilimpenda Judith nae pasina wasiwasi wowote alionesha kunipenda sana.
Kwani pamoja na makazi yangu duni, hakuonekana kushtushwa na kwanza ndio akazidisha mapenzi. Mara kadhaa weekend aliaga kwao nakuja kwangu tukakaa pamoja, tukipika pamoja, tulienda beach na kufurahi pamoja. Kwa kweli nili enjoy sana yale maisha.
Mapenzi yalizidi kushamiri, na nikawa nimezama katika mapenzi na mrembo Judith. Sio siri nilimpenda mno!! Tulipanga mengi kwa pamoja. Tuliahidiana tukimaliza chuo tu baada ya kupata kazi tungeoana na kuanzisha familia. Wazo hili lilipokewa kwa mikono miwili na Judith na akanihakikishia kuwa yupo kwa ajili yangu. Sio siri nilifurahi sana.
Ndugu msomaji, maisha hayatabiriki na muda wowote hubadilika, Tukiwa tunaingia mwaka wa tatu chuoni, Judith alianza kubadilika kidogo kidogo. Hakuwa yule niliemfahamu kwa miaka miwili. Alianza kiburi, kutopokea simu zangu wala kujinijibu sms, na kama angepokea au kunijibu sms basi angefanya kifupi mno. Judith akawa mtu adimu mno kumuona chuoni.
Nilipata tabu mno, hasa ukizingatia jinsi nilivyokua nimezoeana nae. Nikiwatumia rafiki zake wamuulize kama kuna tatizo, lakini sikupata ufumbuzi wowote. Judith alikuwa akinikwepa bila sababu yoyote ya msingi. Nilifanya jitihada zote kurudisha mapenzi yetu katika mstari ila jitihada zangu ziliferi.
Nikapata fununu kuwa Judith anatoka kimapenzi na mkurugenzi fulani wa taasisi ya serikali, zile habari zilikuwa msiba kwangu. Mapenzi yanauma asikwambie mtu.
Hali ilizidi kuwa mbaya kwani nikapata habari zingine kuwa Judith amekuwa top of the town. Anatembea na mapedeshee wa jiji. Na hili halikuwa na pingamizi kwani niliziona picha kadhaa katika mitandao ya kijamii akiwa maeneo tofauti ya starehe.
Baada ya kumsumbua sana kwa kumpigia simu mara kwa mara ndipo alipoamua kunitext na kunieleza ukweli kuwa mimi si chochote, simuwezi, kisa cha kuugua mafua kwa kulala chini nini? Mwanaume huna hata hela ya saloon utanifaa nini? Sio siri ni kama moyo wangu ulisimama ghafla! Nilijuta kuingia ktk mapenz na Judith. Mwanaume nilidondosha chozi.
Kumsahau mwanamke unaempenda ni sawa na kumkumbuka mtu usiemfahamu. Huu msemo ni wa kweli. Nilijitahidi nimsahau Judith na kuendelea na maisha yangu lakini nilipiga hatua mbili na kurudi hatua kumi nyuma.
Nilikonda mno. Sikuwa mlevi ila nikianza kunywa pombe ili nijishaulishe tu lakini haikusaidia kwani kila nilipokuwa nimelewa ningechukua simu yangu na kuanza kumpigia Judith. Pombe haikunisaidia. Nikaachana nayo!
Ni kama Mungu alinipenda tu, kwani pamoja na mambo magumu ya mapenzi nikiyokuwa nikikabiliana nayo, masomo sikuyapa kisogo kwani niliamini ndio mkombozi wa umasikini wangu na familia yangu. Niliomba Mungu anisahaulishe maswahibu yote.
Tulimaliza chuo, na ndio ikawa kama nimepotezana na Judith mazima!! Nikajipa moyo kuwa maisha yanapaswa yaendelee. Jirani na ninapoishi kulikuwa na mzee muuza kahawa niliyekuwa nimezoeana nae sana, huyu mzee alikuwa na shamba ekari moja huko Kijijini. Na alikuwa akiliuza haraka kwani alikuwa na shida ya kumtibia mjukuu wake. Alikuwa akiliuza bei rahisi sana ya Tsh laki tano na nusu. Niliwashirikisha wazazi wangu. Nao wakajichanga changa wakanitumia pesa na kununua plot ile.
Maisha yalisonga, Judith akiwa bado yupo akilini mwangu. Nilihangaika kutafuta kazi huku na huku bila mafanikio. Nilitembea karibia office zote Lakin sikubahatika kupata kazi.
Ni mpaka mwaka mmoja baadae baada ya kusota mtaani ndipo nilifanikiwa kupata kazi katika kampuni ya mafuta na vile vile nikapata taarifa kuwa mradi wa nyumba za kisasa wa Avic town unanunua maeneo huko nje na mji sehemu ambapo na mimi eneo langu nililonunua lipo.
Ekari moja ilikuwa ikinunuliwa kwa Milioni 5, hivyo niliuza ile plot na kupata hicho kiasi cha pesa. Niliwekeza hiyo pesa kwa kufungua mini super market maeneo ya Mji mwema. Pesa nyingine nikanunua kiwanja huko Goba. Na iliyobaki niliwatumia wazazi wangu nyumbani.
Maisha sasa si mabaya. Biashara zinaendelea vizuri na zinastawi kila uchwao. Hii imenifanya niache hata kazi nikiyoipata ili niweze kusimamia vizuri miradi yangu.
Kupitia rafiki zangu nilipata taarifa kuwa Judith alipata ajali wakati akielekea kula bata Arusha na mkubwa mmoja hivi ambae alikuwa ni mume wa mtu. Yule mkubwa alifariki pale pale na Judith alivunjika miguu yote miwili pamoja na mkono wa kushoto. Na zaidi alikutwa akiwa na mimba ya miezi miwili pamoja na HIV+
Nipo hapa nataka niende nikamtembelee kwao, laiti angenisikiliza kipindi kile na kuwa bega kwa bega na mimi tungekuwa mbali hivi sasa. Namwonea huruma kwa maswahibu yaliyomkuta kwani amekuwa mlemavu wa kudumu sasa.
Lengo la ku share na nyinyi story hii ni kuwakumbusha tu, maisha hayana formula. Apangae ni mwenyezi Mungu. Unamdharau mtu kwa kuwa yuko hivi, nakuhakikishia huijui kesho yake. Na kwanini ufanye hivyo? Kwa mamlaka gani uliyonayo hapa Duniani? Kwani wewe hutakufa?
Usikatae akikuita, labda kesho yatakukuta, dunia yabadilika hujui lini atatoka!

Tukutane wiki ijayo............

No comments