Header Ads

Mfahamu Mnyama Twiga

Alichoandika PASCHAL D. LUCAS kuhusu mnyama Twiga

TWIGA ni miongoni mwa wanyama wenye mvuto mkubwa kutokana na uzuri na mambo kadhaa ambayo yanatokana asili yake ikiwa ni zawadi kutoka kwa Mungu… ndio maana hapa nchini Tanzania tunamtumia kama alama ya urithi wa Taifa.

Twiga ni mnyama aliyeambatana na sifa nyingi ukilinganinisha na wanyama wanaopatikana hapa duniani, kwani ni mrefu kuliko wote duniani, ana miguu mirefu,shingo ndefu sana,ulimi mrefu.

Huku sifa nyingine za ziada kutoka kwa mnyama huyu anayeaminika kuwa na maringo kuliko wote ni kuwa na pembe fupi zilizo butu, wakati huo huo mwili wake ukiwa na mabaka yenye rangi ya kahawia-njano na kuzungukwa na rangi ya maziwa.

Mnyama huyu anapatikana katika nyika hususan sehemu zenye migunga, ‘Vkwata’ pamoja na mikakaya,miti ambayo huifurahia sana kwani ndio ni chakula chake kikuu.

Twiga hana ushindani mkubwa wa chakula na wanyama wengine kwa vile yeye hula majani ya juu nchani wakati wanyama wengine hawafikii majani hayo.

Twiga ana urefu wa kati ya mita 4.8 na 5.5 Uzito wake ni kati ya kilo 700 na 1500.Twiga jike ana rangi ng'avu zaidi kuliko dume.Hii inaweza kuwa ni maumbile ya kuwavutia Twiga dume.Dume ni mkubwa na mzito kuliko jike.

Urefu wa ulimi wake ni kati ya sentimeta 46 hadi 50 wakati ambapo urefu wa moyo ni meta 0.6 Ana uwezo wa kukimbia kilometeta 55 kwa saa.Mkia wake ambao ni meta 2.4 ni mrefu kuliko mikia ya wanyama wote duniani.

UZAZI NA MZUNGUKO WA MAISHA.

Twiga hubeba mimba kwa siku 400 hadi  460 , ambazo ni sawa na miezi 14 hadi 15, ambapo mara nyingi huzaa ndama mmoja, huku mapacha ikitokea tu. 

Mama hujifungua akiwa amesimama na kondo lake hukatika mara moja mtoto aangukapo ardhini tofauti na wanyama wengine kama Ng’ombe ambapo huchukua saa kaqdhaa kondo kudondoka.

Ndama akizaliwa huwa na urefu wa mita 1.8 na uzito wa kuanzia kilogramu 40 hadi 70 na Baada ya masaa kadhaa, mama huweza kukimbia japo ndani ya wiki mbili za mwanzo ndama hutumia muda mwingi kujilaza chini huku akilindwa na mama yake kutokana tishio la simba, chui, fisi au mbwa mwitu.

Wanayama hawa wanachangamoto kubwa katika maisha yao wawapo porini kwani ni asilimia 25 hadi 50 na maisha yao mara nyingi huishia kati ya miaka 20 hadi 25 kwa wale Twiga wa mwituni na miaka 28 wale wanaofugwa au kuishi nje ya mbuga.

Kuna nadhalia inayoonyesha kuwa, Twiga wanauhusiano na Tandala,lakini zaidi wamejumuishwa kwenye jamii nyingine ya mnyama Okapi anayepatikana nchi za Amerika, Nigeria na Afrika kusini.

Utafiti wa mwaka 1920 ulithibitisha kuwa twiga hawachangamani na twiga wasio wa kundi moja. Pia pindi dume atakapo kumpanda jike, basi huchagua yeyote aliye katika kipindi cha joto, kwenye kundi lolote. 

Twiga dume hutambua twiga jike walio katika kipindi cha joto kwa kuonja ladha ya mikojo yao.

SHINGO NA NADHALIA ZA MTAANI.

Shingo ndefu ya Twiga imeibua nadhalia nyingi mtaani, ambapo wapo watu wanaodai urefu huo ulitokana na wanyama hao kutaka kuyafikia matawi ya juu ili kujipatia chakula wakati wa ushindani na wanyama wenzao walao majani.

Hata wakati fulani hapa nchinimtu aliyekuwa na uwezo zaidi ndani ya jamii alipewa sifa ya kuwa ni ‘matawi’ ya juu yaani mtu mwenye hadhi ya kipekee kuliko miongoni mwa wanaomzunguka, hususani wanawake warembo.

Lakini wapo wanaoamini kuwa shindo za wanyama hao zinatokana na desturi zao za kusuguana kwa kutumia shingo au madume wanaogombea himaya ya majike kutumia shingo kama silaha ya mapambano.

Kitendo cha kusuguana shingo kwa twiga hufanywa kwa madhumuni mbalimbali, mojawapo ni kupigana vita kali amabapo mara nyingine huwa ni kwaajili ya kutaka kuchukua himaya ya kundi la twiga majike.

Lakini pia kuna siri ambayo watu wengi hawajui kwanini Twiga hususani madume hutumia muda mwingi kusuguana kwa kutumia shingo.

Hakika Mungu alipoumba viumbe vyake kila kimojawapo amekiachia vitu ambavyo aghalabu ni vya tofauti na kipekee sana, kwani Twiga madume yaliyo kwenye upweke hushiriki zaidi zoezi la kusuguana shingo .

Kwa lengo la kutengeneza mihemko na hisia kali za mapenzi hali ambayo mara nyingi huwafikisha kwenye kilele cha mapenzi.
  
MIGUU NA MIONDOKO.
Mara nyingi wanayama hawa wawapo kwenye mazingira yao ya kawaida hutembea kwa madaha na maringo jambo amabalo ukichanaganya na rangi ya miili yao wanavutia sana.

Lakini naomba uelewe kuwa, ikitokea maisha yao yanahatarishwa ikiwemo kutaka kuvamiwa na Simba wanayama hawa huweza kukimbia kwa kasi kubwa mno hadi kufikia umbali wa kilometa 55 kwa saa.

Wakati huo huo Twiga hutumia miguu yake ya mbele iliyo mirefu sana kama silaha hatari ya kummaliza adui yeyote anayejaribu kuhatarisha maisha yake,ikiwemo SIMBA.

Teke la mbele likipigwa linakuwa na nguvu kubwa ya kuweza hata kupasua taya na hata uti wa mgongo wa Simba, jambo ambalo limekuwa si rahisi kwa simba kuwawinda ingawa ndio mnyama pekee tishio kwa twiga.

MFUMO WA MZUNGUKO WA DAMU.
Hapa ndipo pana miujiza ya Mungu, kwani huwezi kufikiria kirahisi kwamba ni kiasi gani damu ya TWIGA inaweza kusafirishwa kutoka kwenye moyo hadi kwenye ubongo kutokana umbali uliopo kati ya viungo hivyo vinavyotenganishwa na shingo ndefu.

Lakini Twiga kawekewa mazingira ya aina yake ya kuhakikisha mfumo wa damu unafanyika bila tatizo lolote licha ya kuwa na maumbile tofauati na wanyama wengine ya kuwa na shingo ndefu inayotenganisha kichwa na moyo.

Kwa haraka haraka ukimwangalia Twiga unaweza kuona kuwa maumbile yake yangeweza kuwa shida katika mfumo wa kusafirisha damu kutokana na tofauti ya umbali kati ya kichwa na moyo,lakini mungu amemuumba Twiga katika 
mazingira yanayomuwezesha jambo hili kufanyika bila shida.


Kwanza moyo wa Twiga unakadiriwa kuwa na uzito wa kilo 10 na urefu wa sentimeta 60, hivyo una uwezo wa kuzalisha mgandamizo wa damu mara mbili ukilinganisha na wanyama wengine.

Hali hii husaidia kuupa nguvu mfumo wa kusukuma damu kwenda kwenye ubongo ulio kwenye kichwa kwa kuwa huwa kipo mbali kutokana na shingo ya mnyama huyo kuwa ndefu sana.

Pia karibu na shingo ya mnyama huyo pia kuna mfumo tata ulioumbwa kwa ajili ya kuminya damu hiyo kwenda kwa wingi kwenye ubongo pindi mnyama huyo anapoinamisha shingo.

MAAJABU YA USINGIZI WA TWIGA.
Twiga ni miongoni mwa mamalia wanaolala muda mfupi zaidi kuliko wote ambapo hutumia wastani wa dakika 10 hadi saa mbili katika saa 24 za siku.

Twiga anaweza kula kilo 29 katika mlo wake kwa siku akisaidiwa na ulimi wake wenye urefu.

No comments