Header Ads

Mtibwa Noma, sare kila kona


Dar/Mikoani. Mtibwa Sugar imefuta uteja wa miaka mitano baada ya kuilazimisha suluhu dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Azam ikishindwa kulinda rekodi yao ya kutokufungwa bao baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Singida United kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
 Vinara wa ligi Mtibwa Sugar mara ya mwisho kupata pointi mmoja jijini Dar es Salaam ilikuwa Februari 2, 2013 ilipotoka sare 1-1 na Yanga. Baada ya hapo imekuwa ikipoteza mechi zake zote.
Katika mchezo wa leo Mtibwa iliyoingia kwa mbinu za kujilinda zaidi shukrani kwa kipa Benedict Tinoco aliyekuwa katika kiwango cha juu.
Tangu kipindi cha kwanza kipa huyo alidaka vizuri na kuokoa hatari nyingi zilizoelekea lango kwake huku akifanya vizuri zaidi dakika 25 za mwisho za kipindi cha pili kwa kuzuia mashabulizi makali ya wachezaji wa Yanga. 
Yanga kama ingekuwa makini ingeweza kupata mabao dakika 25 za mwisho za mchezo baada ya kuingia winga Geofrey Mwashiuya  aliyechukua nafasi ya Raphael Daudi,ambaye aliifanya Yanga ichangamke na kulisakama mara kwa mara lango la Mtibwa Sugar kama nyuki.
Timu zote zilianza mchezo huo kwa kasi zikitafuta mabao ya mapema, lakini safu zote za ulinzi za timu zote mbili zilikuwa makini kuokoa hatari zote.
Katika mchezo huo, Yanga iliwatoa Obrey Chirwa, Raphael Daud, Donald Ngoma na kuingia Thaban Kamusoko na Geofrey Mwashiuya wakati Mtibwa iliwatoa Hassan Dilunga, Salum  Kihimbwa na kuwaingiza  Kelvin Kongwe na Henry Joseph.
 Kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, wenyeji Singida United walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Azam.
Singida United ilikuwa ya kwanza kupata bao  dakika ya 40 kupitia kwa Danny Usengimana baada ya  mabeki wa Azam kuzembea kumkaba na kumlamba chenga kipa wa Azam, Razak Abalora na kuutumbukiza mpira wavuni.
Azam iliendelea kupambanana kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 88 kupitia kwa chipukizi Paul Peter.
Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, wenyeji Ndanda waliichapa Lipuli mabao 2-1.
Mabao ya washindi yalifungwa Asante Kwasi aliyejifunga wakati akijaribu kuokoa shuti lililopigwa na mshambuliji wa Ndanda, Kelvin Friday kabla ya Willium Lucian 'Gallas' kuongeza bao la pili kwa kona iliyokwenda moja kwa moja wavuni. Kwasi alirekebisha makosa na kuipatia Lipuli bao la kufutia machozi kwa faulo.
Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza wenyeji Mbao wamelazimisha sare ya bao 1-1 na Prisons. 
Prisons ilikuwa ya kwanza kufunga bao dakika ya 48, kupitia  Eliuther Mpepo kabla ya Rajesh Kotesha kuisawazishia Mbao dakika ya 84.
Kwenye Uwanja wa Mwadui Complex Shinyanga, Mwadui walilazimishwa sare  ya mabao 2-2 na Mbeya City.
Mbeya City  ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya  kwanza kupitia kwa Mohammed Samatta kabla ya Mwadui kusawazisha dakika 10 baadae kupitia kwa  Evaligestus Bernard kabla ya Bernard kuipatia Mwadui bao la pili, lakini  Mbeya City ilisawazisha dakika ya 79 kupitia kwa  Mohamed Mkopi.
Uwanja wa Mabatini Mlandizi,  Ruvu Shooting ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Njombe Mji. Ruvu Shooting ilipata bao la kuongoza dakika ya 10 lililofungwa na Hamis Mcha kwa penalti kabla ya Gwamaka Kilupe kuisawazishia Njombe Mji.
Kwenye Uwanja wa Majimaji Songea, wenyeji Majimaji wamelazimishwa suluhu na Kagera Sugar.

Wakati huo huo, Simba kesho Jumapili  ina nafasi ya kurejea kileleni  mwa msimamo wa ligi kama itaichapa Stand United katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

Matokeo ya Ligi Kuu Bara
Yanga 0-0 Mtibwa
Singida United 1-1 Azam
Mwadui 2-2 Mbeya City
Ndanda 2-1 Lipuli
Mbao 1-1 Prisons
Majimaji 0-0 Kagera Sugar
Ruvu Shooting 1-1 Njombe Mji

No comments