Header Ads

Arusha yaongoza kwa rushwa


Dar es Salaam. Ukaguzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) mwaka 2016/17 unaonyesha Mkoa wa Arusha unaongoza kwa kuwa na taasisi nyingi zenye viashiria vya rushwa.
Ripoti ya mamlaka hiyo iliyozinduliwa juzi mkoani Dodoma na kukabidhiwa kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ili aipeleke bungeni kujadiliwa imezitaja taasisi 17 zenye viashiria vya rushwa.
Kwenye orodha hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Dk Matern Lumbanga zimo taasisi tano za mkoani Arusha. Pia, kuna mbili za Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwenye orodha hiyo, Dk Lumbanga aliitaja Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Arusha (Auwasa), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Chuo cha Ufundi Arusha, Chuo cha Uhasibu Arusha (AIA) na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Viashiria vya rushwa pia vipo kwenye mikataba ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka ya Moshi (Muwasa) na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro.
Mikoa hii miwili pekee, imetoa theluthi moja ya taasisi zenye viashiria vya rushwa. Waziri Mpango ameshaagiza wahusika wote wa miradi 33 kutoka taasisi 17 zilizotajwa wachukuliwe hatua kwa kupelekwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mikataba 73,154 yenye thamani ya Sh6.31 trilioni ilikaguliwa mwaka 2016/17 kutoka taasisi 185 kati ya 533 zilizotakiwa kufanya hivyo. Kati ya mikataba hiyo; Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Wakala wa Barabara (Tanroads) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) zilipewa kipaumbele.
Taasisi hizo nne zilitumia jumla ya Sh4.65 trilioni sawa na asilimia 73 ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili hiyo.
Licha ya ripoti ya PPRA, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Joseph Haule amezishutumu halmashauri za wilaya za Meru na Ngorongoro kutumia fedha zilizotengwa kwa ujenzi wa barabara kufanya ujenzi wa maabara na utengenezaji wa madawati.
Wakati wilaya hizo zikifanya hivyo, Monduli na Moshi zilifanya malipo kwa kazi zisizofanyika.
Suma JKT
Licha ya Serikali kutaka rushwa ipigwe vita kwenye taasisi zake zote kwa kuongeza uwajibikaji, ripoti hiyo inaonyesha Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa, Suma-JKT kwenda kinyume chake.
Ripoti inabainisha Sh464.46 milioni ‘zimepigwa’ kwenye mikataba miwili ya ukandarasi ambayo Suma JKT imepewa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mwaka 2016/17.
Kwenye mkataba wa kwanza, PPRA inasema NSSF iliitaka Suma JKT kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka Dakawa kwenda Kiwanda cha Sukari kilichopo Mbigiri kwa Sh934.14 milioni lakini Sh366.26 hazina maelezo.
Ripoti inaonyesha waliopewa dhamana NSSF kuilipa Suma JKT walikiuka utaratibu wa ununuzi kwenye mkataba uliohusisha ujenzi wa barabara kutoka Ngerengere kwenda Mkulazi kwa thamani ya Sh1.818 bilioni ambako ubadhirifu wa Sh98.2 milioni umebainika.
Baada ya Rais John Magufuli kuapishwa kuiongoza nchi alibainisha nia yake ya kukomesha ‘upigaji dili’ kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ununuzi wa umma.
Alipendekeza taasisi za umma zipewe kipaumbele ili kukabiliana na udanganyifu unaofanywa.

No comments