Header Ads

Mvua za vuli kuleta mafuriko Arusha


Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imesema mkoa wa Arusha unatarajiwa kuwa na mvua kubwa ambazo zitasababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo.
Mvua hizo za vuli zinatarajiwa kuanza kunyesha Novemba 8 hadi Desemba 28 mwaka huu ambapo msimu wa vuli zinaonyesha kuwa mvua zitakuwa nyingi kuliko msimu uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na TMA ilisema mvua hizo zinatarajiwa kunyesha wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya Arusha Mjini na Vijijini, Karatu, Monduli na Ngorongoro.
Pia TMA ilisema kutakuwa na vipindi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa kusababisha mafuriko na maji yanayopita kwa kasi hivyo wananchi na watumiaji wa pikipiki wanashauriwa kuchukua hatua.
Hatua stahiki zichukuliwe kukabiliana na ongezeko la unyevunyevu ardhini kwani inaweza kusababisha maporomoko ya ardhi yanayotokana na vipindi vifupi vya mvua hizo vinavyoweza kusababisha mafuriko.
“Wakulima wanashauriwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara huku wafugaji watapata malisho ya mifugo na wanyamapor”, ilisema sehemui ya taarifa hiyo
Hata hivyo mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa kunyesha katika wilaya ya Meru na Mashariki mwa Longido hivyo wakulima wanashauriwa kupanda mazao yatakayokomaa kwa muda mfupi.
Kwa upande wa wafugaji wanashauriwa kuvuna, kuhifadhi malisho na maji kwa ajili ya matumizi kipindi cha ukame utakaoanzia Januari hadi Machi mwakani.
Taarifa hiyo ilisema vipindi vya upungufu wa unyevunyevu ardhini unatarajiwa kuathiri uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara pamoja na malisho ya mifugo na wanyamapori.
Hata hivyo taarifa hiyo ilisema ulinganifu wa mvua za vuli zinazotarajiwa kunyesha mwaka huu na msimu uliopita unaonyesha kuwa sawa na msimu uliopita.

No comments