Ukaguzi PPRA waibua mazito
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameagiza maofisa waliohusika na miradi 33 katika taasisi 17 ambazo ununuzi umebainika kuwa na viashiria vya rushwa kupelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru).
Dk Mpango ametoa agizo hilo leo Ijumaa mjini hapa baada ya kupokea ripoti ya tathmini ya utendaji wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Amesema taarifa hiyo ni muhimu kwa sababu fedha za umma zaidi ya asilimia 70 zinatumika kwa ajili ya kununua vifaa na huduma zinazotumiwa na taasisi za Serikali, hivyo watafanya utaratibu wa uwajibikaji kisheria kuwasilisha ripoti hiyo bungeni na atafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa.
Akizungumza kabla ya kukabidhi ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Dk Matern Lumbanga amesema taasisi 81 kati ya 112 zilifanyiwa ukaguzi wa kupima thamani halisi ya fedha.
Pia, mikataba ya miradi 345 ilikaguliwa na kati ya hiyo 87 ilipata alama za kiwango cha kati na saba ilipata alama za kiwango kisichoridhisha.
Amesema katika ukaguzi huo, walibaini malipo yenye utata katika taasisi
tatu ya Sh483.44 milioni zilizolipwa kwa makandarasi lakini hakuna kazi ambazo zilikuwa zimefanyika.
Dk Lumbanga amezitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.
Amesema katika tathmini iliyofanywa na PPRA miradi 33 katika taasisi 17 ilibainika kuwa na kiwango kikubwa cha viashiria vya rushwa ikimaanisha kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa uwepo wa vitendo vya rushwa katika taasisi hizo na miradi hiyo.
Alizitaja kuwa ni mamlaka za maji safi na maji taka Moshi (Muwasa), Mwanza (Mwauwasa), Arusha (Auwasa), halmashauri za wilaya za Msalala,
Kibondo na Moshi.
Nyingine ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela; Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Chuo cha Ufundi Arusha,
Halmashauri ya Mji wa Kahama, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Uhasibu ya Arusha (IAA), Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Mji wa Masasi na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Arusha (AICC).
Kuhusu uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa sheria na kanuni, Dk Lumbanga amesema mwaka jana wa fedha walifanya uchunguzi wa tuhuma nane zilizohusu mikataba 10 ya ununuzi iliyokadiriwa kuwa na thamani ya Sh280 bilioni.
“Uchunguzi huu ulitokana na maagizo kutoka mamlaka za juu au maombi
kutoka taasisi zenyewe,” amesema.
Amezitaja taasisi hizo kuwa ni TRA, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Shirika la Bima la Taifa (NIC),
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga
(TCAA), Wizara ya Fedha na Mipango na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema uchunguzi huo ulibaini taasisi sita za TRA, MOI, Nida, NIC, TCRA na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ziliisababishia Serikali hasara ya Sh12.2 milioni kutokana na sababu mbalimbali.
Sababu hizo amezitaja kuwa ni ucheleweshwaji wa malipo kwa makandarasi uliosababisha ongezeko la riba na faini zilizotokana na ukiukwaji wa
utaratibu wa kijamii na mazingira kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa kazi za ujenzi.
“Kutokana na uchunguzi huo, PPRA iliweza kuingilia kati mchakato wa zabuni tatu zenye thamani ya Sh42.97 bilioni baada ya kujiridhisha kuwa Serikali isingepata thamani halisi ya fedha,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema uchunguzi huo ulibainisha kuwa Serikali ingeokoa takriban Sh1.61 bilioni kama taasisi husika zingetekeleza maelekezo ya mamlaka hiyo.
No comments