Header Ads

Mwigulu Nchemba-Tundu Lissu atasaidia kuwabaini wasiojulikana






Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema kuwa uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu litakuwa la mafanikio makubwa pale ambapo Mbunge huyo atapona na kurejea nchini.
Waziri Nchemba ameyazungumza hayo leo alipokuwa akizungumza katika TV na kueleza kuwa wanaamini Tundu Lissu akipona atakuwa na mchango mkubwa katika kusaidia uchunguzi unaoendelea kufanywa na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi yetu.
“Lissu tunamuombea akishapona atatupa mchango mkubwa wa kusaidia uchunguzi, mtu akiwa kwenye maumivu makali huwezi kumuuliza lolote,” amesema Mwigulu.
Waziri Nchemba amebainisha kuwa uchunguzi unaoendelea teari magari zaidi ya 10 yanayofanana na lililohusika kwenye tukio yamekamatwa na wahusika kuendelea kuchunguzwa.
Aliongeza kuwa baada ya kufanya uchunguzi kwa baadhi ya watu hao waliohusika katika matukio mbalimbali, walibaini kuwa miongoni mwao wapo raia wa Tanzania na wasio watanzania.
Lakini pia amewataka watanzania kuwa na uvumilivu na imani na vyombo vya ulinzi na usalama kwani vinafanya kazi kubwa ya kuilinda amani ya nchi pamoja na kuhakikisha usalama kwa kila raia.
“Hatujui watu wasiojulikana wanapanga nini, ila nawahakikishia Watanzania kuhusu usalama wao.
Tutapambana na mhalifu wa aina yoyote na tutachukua hatua mara moja bila kusita,” amesema.

No comments