Header Ads

Rais Museveni amvika nishani ya heshima Aga Khan

Mtukufu Aga Khan, ambaye ni Imam wa madhehebu ya Ismailia, kupitia taasisi ya Aga Khan ana miradi mingi ya maendeleo katika nyanja za elimu, nishati, afya, hoteli na utalii, vyombo vya habari


Kampala, Uganda.  Rais Yoweri Museveni amemvisha Mtukufu Prince Karim Aga Khan IV nishani ya juu ya heshima barani Afrika (Most Excellent Order of Pearl of Africa, The Grandmaster) ili kutambua miongo kadhaa ya mchango wake katika maendeleo ya Uganda.
Museveni alimvisha nishani hiyo Jumatatu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru yaliyofanyika kwenye viwanja vya Bushenyi-Ishaka katika wilaya ya Bushenyi.
Mtukufu Aga Khan, ambaye ni Imam wa madhehebu ya Ismailia, kupitia taasisi ya Aga Khan ana miradi mingi ya maendeleo katika nyanja za elimu, nishati, afya, hoteli na utalii, vyombo vya habari.
Aga Khan aliwasili nchini Uganda Jumapili kuwahi maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru na alikuwa na kikao na Rais Museveni pamoja na maofisa waandamizi wa serikali katika Ikulu ya Entebbe.
Mapema wakati wa utoaji taarifa kwa waandishi wa habari katika Kituo cha Habari Uganda, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Esther Mbayo alidokeza sababu za kumtunukia nishani hiyo ya heshima Aga Khan.
“Atatunukiwa nishani ya heshima ya juu kwa sababu ya mchango wake mkubwa wa kiuchumi alioutoa kwa nchi yetu duniani kwa ujumla,” alisema Mbayo.

No comments