Profesa Kitila ang’atuka uanachama wa ACT Wazalendo
Dar es Salaam. Profesa Kitila Mkumbo ameng'atuka uanachama wa ACT Wazalendo kuanzia leo.
Ofisa habari wa chama hicho, Abdallah Khamis alipotafutwa ili kuzungumzia suala hilo leo Jumatano amesema kujiondoa kwa mtu kwenye chama au kubaki ni utashi wake.
Barua iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha imesainiwa na Profesa Kitila, imeandikwa kwenda kwa Dorothy Semu, Kaimu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo.
Imeelezwa katika barua hiyo kuwa, “Utakumbuka kuwa nilipoteuliwa kuwa katibu mkuu wa wizara katika Serikali ya CCM nilijiuzulu nafasi yangu ya ushauri wa chama na tukakubaliana kuwa ningeendelea kuwa mwanachama wa kawaida.”
Barua inaeleza hata hivyo, uzoefu wa miezi sita wa kutumikia nafasi yake serikalini umeonyesha ni vigumu kwake kuendelea na uanachama na kutekeleza majukumu yote mawili, yaani ya ukatibu mkuu na uanachama wa ACT Wazalendo bila kuwakwaza viongozi na wanachama.
“Jambo hili limejitokeza zaidi hasa pale ninapotekeleza na kusimamia mipango na mafanikio ya Serikali ambayo mimi ni sehemu yake. Katika mazingira niliyoyaeleza hapo juu, na ili kuepuka mgongano wa wazi wa masilahi (confilict of interest), nimeamua kung'atuka uanachama wangu wa ACT Wazalendo kuanzia tarehe iliyoonyeshwa chini katika barua hii.”
Katika barua hiyo amesema, “Ninakushukuru sana wewe binafsi, kiongozi wa chama, viongozi wengine wa chama na wanachama wote wa ACT Wazalendo katika muda wote tuliofanya kazi pamoja tangu tulipoanzisha chama hiki mwaka 2014 hadi sasa.”
Barua inaeleza atashukuru kukumbushwa kama kuna kifaa au dhamana nyingine yoyote aliyonayo kwa chama ili airudishe.
No comments