NHC Yatoa Kiwanja Kwa Jeshi La Polisi Eneo La Safari City
Na Rashid Nchimbi.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 5000 kwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Polisi na nyumba za askari katika eneo la Matevesi ambapo kuna mradi wa Safari City umbali wa kilomita 12 kutoka katikati ya mji wa Arusha.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi eneo hilo kwa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Masoko wa Shirika hilo nchini Bw. Itandula Gambalagi alisema kwamba, wanatambua umuhimu wa Usalama ndio maana wameamua kutoa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi pamoja na makazi ya askari.
Alisema uwepo wa Jeshi la Polisi katika eneo hilo utawavutia wawekezaji na wakazi wa eneo hilo kuwa na uhakika wa usalama wao na kuliomba Jeshi hilo kuanza kufanya maandilizi ya ujenzi wa kituo hicho kabla ya makazi na maeneo ya biashara hayajafunguliwa.
Akitoa shukrani zake kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba Jeshi hilo litachukua hatua za mapema ili kuweza kujenga kituo hicho ambacho kitaimarisha usalama katika eneo hilo.
“Watu wanaotaka kuwekeza katika eneo hilo wasiwe na shaka juu ya hali ya usalama lakini pia kituo hicho kitasaidia wakazi wa maeneo jirani na kiwanda cha A to Z kilichopo kilomita kadhaa kutoka katika kituo hicho”. Alisisitiza Kamanda Mkumbo
Naye Meneja Mradi wa Safari City Bw. James Kisarika alisema kwamba mbali na maeneo ya makazi pamoja na biashara lakini pia wametenga maeneo kwa ajili ya huduma za jamii kama vile viwanja kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, Misikiti, Makanisa, Shule za Sekondari na Msingi, kituo cha mabasi madogo pamoja na viwanja vya Michezo.
Alisema kwamba mpaka hivi sasa tayari huduma za Maji na Umeme zinapatikana bila shaka yoyote na kuongeza kwamba miundo mbinu ya barabara ipo vizuri.
PICHA NA RASHID NCHIMBI WA JESHI LA POLIS ARUSHA
No comments