Header Ads

Watatu mbaroni kwa kosa la mauaji


Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi imewasomea shitaka la mauaji watu watatu wanaotuhumiwa kumuua kijana Humphrey Makundi aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Scolastica iliyopo Moshi.
Watuhumiwa hao ni mmiliki wa shule ya Scolastica, Edward Shayo mwenye miaka 63, mlinzi wa shule hiyo Hamis Chacha mwenye miaka 28 na Laban Nabiswa mwenye miaka 37.
Upande wa Jamhuri katika shitaka hilo lililofika mbele ya Hakimu Mkazi, Julieti Mawore umewakilishwa na Mwanasheria Kassim Nassiri akisaidiana na Wakili wa kujitegemea, Faygrace Sadallah.
Akisoma maelezo ya hati ya mashitaka mbele ya mahakama hiyo, Nassiri alieleza kuwa mnamo Novemba 6 mwaka huu mshitakiwa wa kwanza, Hamis Chacha wa pili Edward Shayo na wa tatu Laban Nabiswa, walimuua kwa kukusudia mtu aitwaye Humphrey Makundi.

Aidha washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shitaka la mauaji huku akiwataka kusubiri kufanya hivyo pindi watakapofikishwa mahakama kuu ambapo watapata nafasi ya kuwasilisha mashahidi wao pamoja na kujitetea.
Hakimu Mkazi Mawore, ameahirisha shitaka hadi Desemba 8 mwaka huu litakapotajwa tena na  kwamba washitakiwa wote watarudishwa rumande kutokana na  kesi hiyo kutokuwa na dhamana.

No comments