Header Ads

Zitto Atoa Neno Kwa Wanaohama Vyama Kila Kukicha

By, MPEKUZI

KWA MUJIBU WA MPEKUZI.COM
Kufuatia vuguvugu la hivi karibuni  la wanasiasa kuhama vyama vyao na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) huku wengine wakitoka CCM na kuhamia upinzani, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameamua kutoa ya moyoni kuhusiana na sarakasi hizo za kisiasa.

Katika chama chake cha ACT-Wazalendo, Zitto amepoteza wanasiasa kama Samson Mwigamba, Dkt. Kitila Mkumbo na wanachama wengine 10 ambao wametimkia CCM huku aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Mama Anna Elisha Mghwira akijiuzulu nafasi hiyo na kusalia kuwa mwanachama wa kawaida baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto ameandika yafuatayo;

“Kuhama au kubadili Chama cha Siasa sio jambo geni katika siasa zetu, na ni haki ya kikatiba ya Mtanzania yoyote kufanya ivyo. Kitu cha msingi ni kitendo hicho kuongozwa na imani thabiti kwenye misingi ya chama unachokwenda.

Siku zote ninaamini kuwa vyama vinapaswa kujengwa juu ya misingi ya Itikadi. Sisi ACT Wazalendo itikadi yetu imejengwa kwenye Azimio la Tabora kuhusu Siasa ya Ujamaa wa Kidemokrasia. Tutaendelea kufanya siasa za masuala na kuimarisha mfumo wa Vyama vingi nchini kwetu.

Mimi Binafsi na Wanachama wenzangu wa ACT wazalendo tunawatakia heri na mafanikio wenzetu waliojiunga na vyama vingine. Sisi wengine tutaendelea kujenga Vyama kama Taasisi muhimu za Maendeleo katika Nchi yetu. Kamwe hatuwezi kuruhusu nchi yetu kuwa ya chama kimoja. Kwa mazingira ya kisiasa ya sasa, kuwa mwanachama wa Chama cha Upinzani ni uzalendo uliotukuka.

Ni dhahiri kuwa Chama kuondokewa na wanachama wake sio jambo jema. Lakini ukitazama watu wanaohama vyama ni wanasiasa wale wale wa siku zote na walikuwa kwenye vyama vingine kabla na kuhamia vyama wanavyotoka sasa. Kwangu mimi kuna somo moja kubwa nalo ni kuandaa aina Mpya ya wanasiasa, wanasiasa wanaojengwa kwenye itikadi na misingi. Kazi kubwa iliyopo mbele yangu kama Kiongozi ni kuandaa kizazi kipya cha Viongozi wa kisiasa wajamaa. Hiyo ndio kazi ninayofanya sasa. Forward Ever, Backward Never.”

Zitto Kabwe, Mb
Mtwara
23/11/2017.

No comments