Header Ads

RAIS MAGUFULI AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KULIOMBEA TAIFA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli leo tarehe 17 Desemba, 2017 wameungana na waumini wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma kusali ibada ya Jumapili.
Akizungumza baada ya Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote wa dini na waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini kwa kuendelea kuliombea Taifa ili lidumishe amani na upendo.Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali anayoiongoza inatambua juhudi zinazofanywa na viongozi wa Dini katika kudumisha amani na upendo na ameahidi kuwa itaendelea kushirikiana nao katika kujenga Tanzania bora.“Nawaomba viongozi wa madhehebu yote ya dini tuendelee kuliombea Taifa letu liwe na amani na upendo, na Serikali itashirikiana nanyi muda wote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Padre wa kanisa hilo Fr. Sergio Madinda amemshukuru Mhe. Rais kwa ushirikiano wake na kanisa na pia amemshukuru kwa uamuzi wake wa kuhamishia Serikali Dodoma.Katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa Shilingi Milioni 3 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Kigango cha Michese na kwaya ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba.

Gerson Msigwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULUDodoma17 Desemba, 2017

No comments