Header Ads

AFISA KILIMO AUWAWA NA MAJAMBAZI SHINYANGA



Afisa kilimo kata ya Bukene – Didia wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ndonho mwenye umri wa miaka 32, ameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi waliokuwa wanavamia duka la Juma Mnyesi miaka 47 katika kijiji na kata ya Didia wilayani humo.
Akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule amesema mauaji hayo yametokea jana Januari 23,2018 saa mbili na dakika 40 usiku katika kijiji cha Didia, kata ya Didia, tarafa ya Itwangi, wilaya ya Shinyanga vijijini na mkoa wa Shinyanga.
Kamanda Haule amesema afisa kilimo huyo wa kata ya Bukene – Didia aliuawa kwa kupigwa na risasi ya bunduki aina ya AK 47/SAR sehemu za paji la uso na kisha kutokea kisogoni na kutokwa na damu nyingi na kusababisha kifo chake papo hapo.
“Chanzo cha mauaji hayo ni kuwania mali kwani hapo awali marehemu alikutana na watu wanaokadiriwa kuwa watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za moto na mapanga waliokuwa katika harakati za kwenda kuvamia katika duka la Juma Mnyesi mfanyabiashara wa Didia”, ameeleza Kamanda Haule.
“Katika tukio hilo Juma Mnyesi na mke wake aitwaye Mariam Lukuba (47) walijeruhiwa kichwani kwa kitu chenye ncha kali na kisha kuchukuliwa pesa za mauzo ya dukani shilingi milioni 2”,ameongeza Kamanda Haule.
Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa uchunguzi zaidi na majeruhi wamelazwa katika kituo cha afya Bugisi na hali zao zinaendelea vizuri.
Ameongeza kuwa katika eneo la tukio ziliokotwa risasi mbili (Misfire ) na maganda ya risasi 11 za bunduki aina ya AK 47/SAR.
Kamanda Haule anawaomba wananchi wote mkoani Shinyanga kusaidiana na jeshi la polisi kutoa taarifa kuhusiana na waliohusika katika mauaji na uporaji huo ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akiwa katika kijiji cha Didia baada ya tukio la mauaji kufanyika

No comments