BWENI LATEKETEA KWA MOTO MWANZA
Jengo la bweni la wanafunzi wa kiume katika shule ya Sekondari Katunguru wilayani Sengerema mkoani Mwanza limeteketea kwa moto.
Kwa Mujibu wa Mwananchi kuteketea kwa jengo hilo lililogawanywa katika sehemu tatu kumewakosesha malazi wanafunzi zaidi ya 200 wa shule hiyo.Mkuu wa shule hiyo, Baraka Msimba amesema moto huo ulianza saa tatu usiku wa kuamkia leo.“Hadi sasa hasara iliyosababishwa na moto huo inakadiriwa kuwa zaidi ya Sh70 milioni,” amesema Msimba na kuongeza: “Hakuna mali ambayo imeokolewa ikiwemo madaftari, vitabu, magodoro, blanketi, mashuka na nguo za wanafunzi.Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Sengerema, Magesa Mafuru amesema ofisi yake inafanya kila linalowezekana kuwasaidia wanafunzi hao ili waendelee na masomo.“Wakati halmashauri ikiendelea na juhudi za kurejesha hali ya kawaida shuleni hapo, naiomba jamii kila mmoja mwenye uwezo kujitokeza kuwasaidia wanafunzi hawa kuendelea na masomo na maisha ya kawaida,” amesema Mafuru.
No comments