Header Ads

MAJINA YA ASKARI 11 WALIOSIMAMISHWA KAZI.

Jeshi la Magereza nchini limewasimamisha kazi askari wake kumi na moja waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya mwanakijiji, Aloyce Makalla (41) mkazi wa kijiji cha Kerenge wiki iliyopita.Taarifa za ndani ya jeshi hilo zinasema askari hao walisimamishwa kazi na Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa juzi.Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, John Masunga alithibitisha kusimamishwa kwa askari hao lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi kwa kuwa msemaji wa jeshi hilo ni Kamishna Jenerali pekee na si mtu mwingine.
Askari waliosimamishwa baada ya  kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Korogwe  Tanga mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kassim Mkwawa ni Jonas Makere, Shadrack Lugendo, Lazaro Stephen, Mussa Zuberi, Ramadhan Yusuf, Robert Alfred, Fhidirish Osmas, Alfonce Revocatus, Mbesha Naftari, Hamis Msola na Michael Elias.
Hatua ya kuwasimamisha kazi askari hao imechukuliwa ikiwa ni kupisha vyombo vya sheria kufanya kazi yake kwa uhuru zaidi na hatima yao itategemea uamuzi wa mahakama hiyo.
Kutoka mahakamani inadaiwa mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Saraji Iboru kuwa Januari 22, 2018 saa 9.30 katika kitongoji cha Mapangoni Kijiji cha Kerenge, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua mwanakijiji huyo.
Saraji Iboru ambaye alikuwa akisaidiana na mwendesha mashtaka kiongozi, Shosa Naiman alidai kwamba siku ya tukio, washtakiwa hao walikwenda nyumbani kwa Makalla wakimtuhumu kwamba Januari 15, 2018 alimjeruhi askari mwenzao aitwaye Sajenti Stephen.Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji. Hakimu Mkwawa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 15 itakapotajwa tena.

No comments