Header Ads

MGODI WA GGM WAPEWA SIKU MBILI

Wizara ya Madini imetoa muda wa siku mbili kwa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), kukamilisha mchakato wa ulipaji fidia nyumba zaidi ya 80 za wananchi zilizopata nyufa kutokana na milipuko inayosababishwa na ulipuaji wa miamba.
Wananchi wa Nyamalembo wanaoishi jirani na mgodi huo wamekuwa wakilalamika kwa zaidi ya miaka mitano kuhusu nyumba zao kupata nyufa kutokana na mitetemo inayosababishwa na milipuko, huku Serikali ikiagiza mara kwa mara mgodi kuwalipa fidia bila utekelezaji.
Akizungumza juzi na wananchi wa Nyamalembo na Katoma wanaozunguka mgodi huo, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema madai ya wananchi sasa yamefika mwisho.
Alisema migogoro mingi katika sekta ya madini kuna uwezekano inasababishwa na upungufu wa kisheria.
Nyongo alisema licha ya sheria na kanuni mpya kutungwa, bado zipo sheria zinasababisha matatizo kwa wananchi.
“Tunataka mwananchi muone maendeleo ya kuwa na mwekezaji katika maeneo yenu na hatuoni sababu ya mwekezaji kuwa kero kwa wananchi,” alisema.
Pia, aliwataka wawekezaji kutotumia udhaifu wa kisheria kuwakandamiza wananchi.
“Kuna watu wanajua sheria na wanatumia udhaifu wa sheria zetu kumkandamiza mwananchi, sisi hatutasita tutakuwa nyuma ya wananchi kuhakikisha wanapata haki zao.
Haya malalamiko ya wananchi yameanza kabla ya mwaka 2010, lakini hadi leo hakuna utekelezaji, hatutasita kukuchukulia hatua wewe unayetumia udhaifu wa sheria kumkandamiza mwananchi,” alionya naibu waziri.
Nyongo aliutaka mgodi huo kuwalipa fidia wananchi wa Mtaa wa Katoma wanaoishi ndani ya leseni za mgodi na kama hawako tayari kulipa wawaache waendeleze shughuli zao.
Vilevile, aliitaka halmashauri kuwapa wananchi hati za ardhi ili waweze kupatiwa huduma ya maji na umeme.Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti, Simon Shayo alisema masuala mengi yanayolalamikiwa yapo kisheria na kuomba yatizamwe kwa mujibu wa sheria ili haki itendeke kwa pande zote mbili.
Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu alisema changamoto kubwa kwa GGM ni washauri wa mgodi kupotosha viongozi wao juu ya ulipaji wa fidia na kusababisha wananchi wanaozunguka mgodi huo kuendelea kuteseka kwa kukosa huduma za maji na umeme.Kanyasu alisema licha ya taarifa za mgodi kuonyesha wanalipa asilimia 0.5 ya pato la Taifa, bado maisha ya wananchi wa Mji wa Geita hayaendani na hali halisi ya utajiri wa dhahabu iliyopo.
Katibu wa kamati iliyoundwa na wananchi wa mitaa ya Katoma na Nyakabale, Jackson Mabula alimuomba naibu waziri kusimamia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais John Magufuli, mawaziri na naibu mawaziri ili kuondoa mgogoro baina yao na GGM.

No comments