Header Ads

ARUSHA DC YAJIPANGA KUMWINUA MWANAMKE KIUCHUMI

Kila ifikapo Machi 8 kila mwaka huwa ni siku ya wanawake duniani kote.

Kwa hapa nchini Kauli Mbiu ilikuwa "Kuelekea Uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini." 

Hivyo basi siku ya Wanawake Dunia watu mbali mbali wamekuwa na la kuzungumza katika siku hiyo muhimu.

Lakini kwa upande wa Wilaya ya Arusha Dc maadhimisho hayo yaliadhimishwa kwa maonyesho mbalimbali ya kina mama (wanawake ) kwa kuonesha vipaji na namna wanavyoweza kuinua jamii kiuchumi.

  Katika maadhimisho hayo Wanawake wameonesha kuwa chachu na hamasa ya kuunga mkono suala la uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo ambavyo huwaingizia kipato.Na mpaka sasa Arusha DC kwa sasa asilimia 60% ya viwanda vidogo vinamilikiwa na wanawake.

Katika kutekelezaWanawake wametakiwa kujikita zaidi  kwenye uzalishaji wa malighafi na bidhaa za viwanda, vitakavyowawezesha kujiajiri katika kuelekea uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.

Kwa upande wa  Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC imejipanga kuwainua na kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji ili kuwasaidia  wanawake kuinua viwanda hivyo kuelekea viwanda vya kati hadi vikubwa katika uchumi wa viwanda.

  Halmashauri yaArusha DC imejipanga kukusanya mapato yake ya  ndani kwa lengo la kupata  asilimia 4% ya kuwakopesha wanawake, na kuwataka wanawake hao kulipa kodi na ushuru wa bidhaa zao ili kuwezesha halmashauri kupata mapato yake ya ndani ili iweze kujiendesha na kusaidia nguvu za mwanamke katika kujikwamua kiuchumi.

Nayo idara ya Maendeleo ya Jamii imetakiwa kuwaunganisha Wanawake wajasiriamali ili wazalishapi bidhaa zao ziweze kusajiliwa na kupatiwa vibali vya viwango vitakavyowezesha bidhaa zao kupata soko ndani na nje ya Tanzania.

Pamoja na hayo yote changamoto za kumwinua mwanamke haziwezi kukosekana hivyo halmashauri  imejikita katika kutatua changamoto za wanawake ikiwemo kuboresha hali za uchumi kwa kutoa mikopo, kuboresha sekta za elimu kwa kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu, kuboresha miundo mbinu ya huduma za afya kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuboresha huduma za maji kwa kutekeleza miradi mingi ya maji ili kumpunguzia mama mzigo wa kuchota maji na kutekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano.

Kwa upande wa viongozi wamekiri kupambana na mila kandaamizi dhidi ya wanawake na kuthibitisha kuwa ukeketaji wa watoto wa kike umepungua kwa kiasi kikubwa zaidi na unaelekea kuisha kabisa hivyo basi viongozi wameamua kulinda na kutetea masilahi ya wanawake ili kuwa na taifa lenye nguvu na kujiamini dhidi ya mwanamke.

Katika kumwinua mwanamke kiuchumi na dhidi ya manyanyaso ayapatayo  katika familia dunia inatambua changamoto zinazowakabili wanawake zinazotokana na  wanaume kukwepa majukumu, lakini Mungu anasikia kilio cha wanawake na kutambua kuwa wanawake ni jeshi kubwa na lenye ushawishi, hivyo wanatakiwa kuungana na kufanya ushawishi wa maendeleo ya taifa la Tanzania.

Hivyo basi wanawake wametakiwa kuwa na nidhamu ya mikopo pamoja na kujenga tabia ya kujiwekea akiba katika benki jambo ambalo litawawezesha kupata mikopo mikubwa zaidi pindi biashara zao zitakapokuwa kubwa.

Kitaifa maadhimisho ya mwanamke duniani yameadhimisha mkoani Dar Es Salaam huku yakiongozwa na mke wa rais Mama Janeth Magufuli.

Kauli Mbiu: "Kuelekea Uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini."

No comments