Header Ads

WANANCHI WAPANDA ZAIDI YA MITI 5000 WILAYANI ARUSHA.

Katika kuazimisha siku ya upandaji miti kitaifa inayoambatana na kauli mbiu ya  'Tanzania ya kijani inawezekana.
Halmashauri wilaya  ya Arusha imezindua rasmi siku ya upandaji miti kiwilaya ambapo maadhimisho ya uzinduzi  huo kiwilaya yalifanyika katika kata ya Ilkiding'a mkoani Arusha.
Akiwa katika uzinduzi huo mgeni rasmi ambaye pia ni Afisa Utumishi wa halmashauri ya wilaya ya  Arusha, Bw.Selemani Sekiete alisema kuwa, halmashauri imeandaa mkakati thabiti wa kupanda miti kwenye maeneo yote  ndani ya wilaya  kwa kutoa miche ya miti kwa taasisi na watu binafsi bila malipo kutoka kwenye kitalu cha miti cha halmashauri.
Bw.Sekiete aliongeza kuwa licha ya kutoa miche hiyo bure pia watalamu wa masuala ya miti na misitu watatoa ushauri na mafunzo juu ya uoteshaji na utunzaji wa miti hiyo.
Aidha amefafanua kuwa kwa sasa, wananchi wanapaswa kupanda miti kama zao la biashara, zao linaloruhusu na ufugaji wa nyuki katika miti hiyo na kuwataka vijana kujikita katika upandaji wa miti katika maeneo yao.
Bw.Josephat Likindambeki mwanakijiji aliyeshiriki zoezi la upandaji miti, amethibitisha kupatiwa miche bure na kusema kuwa jambo hilo linawahamasisha wananchi kupanda miti na kufahamu umuhimu wa kupenda kutunza mazingira yao.
"Zamani sikufahamu umuhimu wa kupanda miti wala kutunza mazingira, nilipokwenda halmashauri kuomba miche wakanishauri na kunielekeza aina ya miti ya kuotesha na umuhimu wake kwa mazingira" alisema Likindambaki.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Afisa Wanyamapori halmashauri ya Arusha, Tabea Mollel amesema kuwa kitengo cha Maliasili kimepanga kupanda miti zaidi ya milioni 2.5 kwa mwaka huu pamoja na uhamasishaji wa ufugaji wa nyuki katika miti hiyo ili kupata malighafi za viwanda zitakazotokana mazao ya miti na nyuki.
Hata hivyo Mollel amesema kuwa licha ya jitihada za kupanda miti kwa wingi bado miti hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukame kwa baadhi ya maeneo na mifugo kwa maeneo ya wafugaji, changamoto inayopoteza zaidi ya aslimia 30% ya miti inayopandwa kila mwaka.
Ameongeza kuwa, licha ya changamoto hizo bado wanaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kufanya ufugaji wa kisasa wenye tija wa kutumia eneo dogo ili kutunza mazingira  na kuwa na mifugo michache na kupunguza uharibifu wa mazingira.

No comments